Home KITAIFA TIMU YA MAWIZIRI KUONGEZA NGUVU RUFIJI,KIBITI-MAJALIWA

TIMU YA MAWIZIRI KUONGEZA NGUVU RUFIJI,KIBITI-MAJALIWA

Na Mwandishi wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Timu ya Mawaziri itakwenda wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani kuungana na timu ya watalaam ili kufanya tathmini ya pamoja kutokana na athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokea wilayani humo.

Ametoa kauli hiyo leo Aprili 09, 2024 wakati wa hafla ya Futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma.

“Sisi ndio tunaratibu Idara ya Maafa kitaifa, hapa tunapozungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama pamoja na Katibu Mkuu Dk. Jim Yonaz wako njiani wanaelekea mkoani Pwani, mto rufiji umejaa na kata nne zipo kwenye maji, mawaziri wengine wa sekta ikiwemo afya, kilimo, mifugo nao pia wanakwenda ili kuimarisha uratibu wa zoezi,”amesema Majaliwa.

Pia Waziri Mkuu ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namna inavyodhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.

“Kamishna amefanya kazi nzuri na kuboresha kwenye sekta yake, hivi sasa taasisi yake haiishii tu Makao Makuu ya nchi, ameshusha kwenye kanda na tayari wakurugenzi wameshaenda kwenye maeneo hayo ambao watakamata wazalishaji, wasafirishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya,”amesema.

Viongozi wengine walioshiriki katika iftar hiyo ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here