Home KITAIFA Dk.Gwajima amesema taasisi mbalimbali nchini kuendelea kuwekeza kwa wanawake

Dk.Gwajima amesema taasisi mbalimbali nchini kuendelea kuwekeza kwa wanawake

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima ametoa rai kwa taasisi mbalimbali nchini kuendelea kuwekeza kwa wanawake, kwani kwa kufanya hivyo, ni kuongeza kasi ya maendeleo, kukuza Ustawi wa jamii, na kujenga familia bora kwa maslahi ya Taifa .

Wito huo ameutoa leo March 6,2024 jijini Dar es salaam kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo ya mwanamke kiongozi awamu ya tisa yaliyoratibiwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) ambapo yamelenga kuwajengea uwezo wanawake kumudu nafasi za juu za uongozi.

Amesema wanawake ndio msingi mkubwa wa maendeleo katika ngazi tofauti kuanzia familia hadi Taifa hivyo kuwekeza kwa mwanamke ni kuliendeleza Taifa.

“Wanawake tushiakamane,na ninyi mliopo maeneo ya kazi, muwanyanyue na wengine, muwasaidie ili na wao watimize malengo yao msiwe visababishi vya misongo ya mawazo kwa wengine,”amesema Dk.Gwajima.

Aidha amewataka wanawake ambao wamehitimu mafunzo hayo na wapo kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kuhakikisha wanawasaidia wanawake wengine.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na ATE kuhakikisha kunakuwa na rafiki ya ushiriki wa wanawake katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, ili kukuza uchumi wa nchi na wananchi wote.

Akizungumzia Kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia ametoa wito kwa jamii kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo lakini pia kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kuwalinda wanawake na watoto, huku akisisitiza mitandao itumike kuleta tija kwa jamii.

Dk .Gwajima amesema Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Wanawake (UN Women), limeeleza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake hugharimu asilimia mbili ya uchumi wa dunia na Ripoti ya Benki ya Dunia kionyesha baadhi ya ya nchi hutumia hadi asilimia 3.5 ya Pato Taifa la ndani kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia.

“Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba, hatutaweza kusonga mbele ikiwa tutaendelea kufumbia macho masuala haya,”amesema.

Naye Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewahasa wanawake pamoja na kuwa na nafasi mbalimbali katika uongozi wasiache jukumu la malezi ya familia kwa kuwalea watoto na kuwafundisha maadili na uzalendo.

Amesema Mmomonyoko wa maadili kwa vijana unatokana na usimamizi mbaya na malezi ya wazazi kwa kuwaachia majukumu ya malezi wafanyakazi wa nyumbani(House girl)

Katambi amesema taifa linakosa viongozi kutokana na mmomonyoko wa maadili akidokeza wazazi kuwa “busy” na mambo yao badala ya kujali makuzi na malezi ya familia.

“Usiwaachie wasaidizi wa ndani kuwa wazazi,wanawake mliopo hapa ujuzi na maarifa mliopewa, fedha tunazotafuta nyumba na magari hazina maana, takwimu nilizonazo watoto wengi wa viongozi wanaharibikiwa sana hata nafasi za ajira zikitoka hawataki kujituma wanakwenda kusema baba amenituma,”amesema Katambi.

Amesema watoto wamekuwa wakilawitiwa kutokana na ubize wa wazazi kutokana na kuwaachia wasaidizi wa ndani kila kitu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk.Suzan Ndomba amewataka wanawake waliopewa mafunzo ya uongozi kutumia maarifa waliyopewa kuleta mabadiliko na kuwabadilisha wengine kwa ustawi wa Taifa na maendeleo endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here