Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeweka mfumo madhubuti wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi itakayotekelezwa kupitia fedha za Zanzibar Sukuk.

Ameeleza hayo leo Aprili, 29 2025 alipoifunga Awamu ya Kwanza ya Uwekezaji wa Hatifungani ya Zanzibar Sukuk Hafla iliofanyika Viwanja vya Ikulu , Zanzibar.
Dk. Mwinyi amesema fedha zilizopatikana zitapelekwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo yenye tija ikiwemo miradi ya miundombinu ya barabara Unguja na Pemba ,bandari jumuishi ya Mangapwani , Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Binguni na kumaliza kazi ya Ujenzi wa Jengo la Abiria la Terminal 2 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Ameeleza kuwa mafanikio yaliopatikana katika Awamu ya Kwanza ya Zanzibar Sukuk yameifanya Zanzibar kuwa kituo cha kujifunzia kwa nchi za Afrika Masharti na baadhi ya nchi za Afrika katika uendeshaji wa mpango huo.
Dk.Mwinyi amesema mafanikio hayo yameonesha dhamira thabiti ya Serikali ya kuwa na uchumi jumuishi unaowashirikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza.

Aidha amefafanua kuwa kwa mafanikio hayo hivi karibuni Serikali inakusudia kuanzisha Soko la Mitaji la Zanzibar yaani (Zanzibar Securities Exchanges) ambalo pia litasaidia kupatipakna kwa mitaji ya kuwekeza katika biashara mbalimbali pamoja na miradi mikubwa ya Serikali hatua alioielezea kuwa ni Muhimu kufikia lengo la Nchi kuwa ni Kituo cha Fedha (Financial Hub).ś0
Rais ameipongeza Wizara ya Nchi ,Afisi ya Rais Fedha na Mipango na Taasisi ya Ufuatiliaji wa Mipango ya Serikali (PDB) kwa kufanikisha mpango huo kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri na kuwataka Kuendelea kuwa Wabunifu zaidi kuibua njia Mbadala za kutafuta fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo .
Aidha amewapongeza wawekezaji wote waliowekeza katika awamu hiyo ya kwanza na kuwasisitiza kufanya hivyo katika awamu nyingine ili kuunga mkono juhudi za Serikali .

Amewahakikishia Wawekezaji hao kuwa mapato ya kila mwaka ya asilimia 10.5 na Yale ya asilimia 4. 2 kwa wanaowekeza kwa dola pamoja na fedha za mitaji zilizowekezwa kila baada ya miaka saba yatapatikana kwa wakati kama ilivyoainishwa katika masharti ya mpango huo.
Rais Dk.Mwinyi amewasisitiza Wananchi kudumisha amani na Mshikamano kwani bila ya kuwepo Amani hakuna Mafanikio ya Aina hiyo yanayoweza kupatikana.
Naye Waziri wa Nchi Afisi ya Rais ,Fedha na Mipango Saada Mkuya Salum amesema zaidi ya shilingi bilioni 381 sawa na asilimia 128.33 zimewekezwa katika Awamu ya Kwanza ya Zanzibar Sukuk na kuvuka makadirio ya awali ya shilingi bilioni 300.