Zaidi ya shilingi Bilioni 432 zimewekezwa ununuzi vifaa vya kisasa na mifumo
•Siku za kuondosha mskasha zimepungua kutoka siku 40 hadi siku 0 au 3
•uingizaji makasha umevunja rekodi makasha 1,000,000 kwa mwaka na kuwa bandari bora
•Makaa ya mawe ni fursa ya biashara kupata fedha za kigeni na Nishati ya viwanda vikubwa
Masasi
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa uboreshaji wa Bandari ya Dar es salaam kupitia kampuni ya DP World umeongeza mapato , idadi ya makasha yanayoingia na kupungua kwa siku ya meli kukaa bandarini

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ameeleza hayo leo Aprili 17,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ikiwa ziara yake ya siku kumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makalla ameeleza hayo akijibu hoja ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche aliyedai kuwa Nchi yetu imeshindwa kuendesha bandari na kuwapa watu binafsi.

Amesema mtoa hoja hajui mambo ya uchumi na Biashara anahitaji aelimishwe faida za uwekezaji na uboreshaji bandari ya Dsm ambayo imekuwa moja ya bandari yenye ufanisi Afrika mashariki na kati.
Pia amesema kuwa makaa ya mawe kuuzwa nje ya nchi ni fursa nzuri inayosaidia serikali na taifa kwa ujumla kuongeza mapato na fedha za kigeni zinazosaidia kufanya maendeleo ya nchi kutokana na masoko yanayopatikana nje ya nchi.
“Kuwa na makaa ya mawe ni fursa kwa sababu yanatumika katika kazi mbalimbali na hapa ndani ya nchi uhitaji wa makaa ya mawe ni mkubwa katika kwenye viwanda vyetu,” amesema Makalla.

Ameongeza: “Kwahiyo namwambia John Heche mbali ya kupata fursa ya masoko nje ya nchi na kutuingizia fedha za kigeni ambazo tunazipata na tunapata kodi yetu na Rais anapata uwezo wa kujengo shule, kuweka miradi ya maji na kujenga barabara nk”
Pia Makalla amesema kuwa Tanzania makaa ya mawe yanatoka kusini na kuna viwanda vya saruji nchini ambavyo vinahitaji uwepo wa makaa ya mawe kikiwemo kiwanda cha saruji cha Wazo, Tanga Cement na cha Dangote vyote vinauhitaji wa malighafi hiyo.