Dar es Salaam
BODI ya Uwekezaji na Fedha ya Watumishi Housing Investment (WHI) ,imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba 101 unaotekelezwa katika eneo la Mikocheni, mkoani Dar es Salaam, ambao ujenzi huo hadi kukmilika kwake kugharimu shilingi bilioni 18.

Ziara hiyo iliyofanyika leo Aprili, 17 2025 jijini Dar es Salaam na wajumbe wa bodi hiyo walionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na viwango vya ubora vinavyotumika katika ujenzi.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Celestine Muganga, amesema mradi huo umejengwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa umma na tayari nyumba zote zimekwishalipiwa.

“Tunatambua kuwa mahitaji ya makazi ni makubwa. Tayari eneo hili limekwishalipiwa lote. Tumejionea utekelezaji wenye tija unaoendana na malengo ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watumishi na wananchi wanapata makazi bora na salama,” amesema Muganga.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Sephania Solomon, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 26, 2026 hukulikiwa ni kuondoa changamoto ya makazi, hususan kwa watumishi wa umma wa kipato cha kati na cha chini.
“Nyumba hizi zimebuniwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, mazingira rafiki na bei nafuu. Tumeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuwawezesha wanunuzi kupata mikopo kwa masharti nafuu, hivyo kuwasaidia kumiliki makazi yao kwa urahisi zaidi,” amesema Solomon.

Naye Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Yusuph Mlimakifu, amesema ujenzi huo unaohusisha nyumba zenye chumba kimoja, viwili na vitatu umefikia asilimia 20. Alieleza kuwa hadi sasa hakuna changamoto kubwa na wanaendelea na kazi kwa kasi ili kukamilisha mradi kwa wakati kama walivyopanga.
Watumishi Housing Investment imeendelea kutekeleza miradi ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mtanzania anapata haki ya msingi ya makazi bora.