Home KITAIFA TASAC YAWAJENGEA UWEZO MAWAKALA WA MELI, FORODHA NA WAKUSANYAJI NA WATAWANYAJI WA...

TASAC YAWAJENGEA UWEZO MAWAKALA WA MELI, FORODHA NA WAKUSANYAJI NA WATAWANYAJI WA MIZIGO MWANZA

Mwanza

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 16 Aprili, 2025 limeendesha mafunzo kwa wadau wa usafirishaji mkoani Mwanza wanaojishughulisha na shughuli za uwakala wa meli, uwakala wa forodha, wakusanyaji na watawanyaji wa mizigo katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya TASAC jijini Mwanza.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Meneja Udhibiti Huduma za Usafiri Majini, Fatuma Masenene amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuchagiza uwezo wa watoa huduma ili waweze kutoa huduma stahiki kwa ufanisi, tija na ushindani wa kiwango cha kimataifa.

Amesema kuwa kwa muda mrefu TASAC, kwa niaba ya Serikali, imetamani kuona wadau wa usafiri majini hapa nchini wakiendelea kujengewa uelewa kuhusu namna bora ya kufanya biashara kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji.

“Sekta ya usafiri majini ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla. Kwa mujibu wa takwimu za UNCTAD, zaidi ya asilimia 90 ( kwa uzito) ya shehena inayouzwa kimataifa husafirishwa kwa njia ya maji,” amesema Masenene.

Ameongeza kuwa TASAC imelenga katika kuendeleza ushirikiano kati yake kama mdhibiti na wadau wa sekta inayodhibitiwa kama njia mojawapo ya kuinua uchumi kupitia sekta ya usafiri majini.

“Kupitia mkutano huu tutajifunza kuhusu utaratibu na masharti ya leseni za mawakala wa meli na wakusanyaji na watawanyaji wa mizigo midogo midogo; na utaratibu na masharti ya kupata vyeti vya usajili kwa mawakala wa forodha,” amesema Bi. Masenene.

Akizungumza kwa niaba ya wadau waliohudhuria mafunzo hayo, Anselm Namala Mkuu Masoko na Uhusiano kwa Umma Kampuni ya Meli (TASHICO) ameipongeza TASAC kwa kuwajengea uwezo na kusema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kuboresha kazi zao na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaotegemea kupata huduma kutoka kwao.

“Tunapojengewa uwezo sisi wasafirishaji, mawakala wa uhakiki mizigo, mawakala wa forodha, na mawakala wa meli na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama maeneo ya bandari tunakuwa katika nafasi ya kuhakikisha kwamba mzigo wa mteja unakuwa mahala salama na unafika katika hali nzuri kama anavyotegemea, hivyo yatasaidia kuboresha huduma kwa wateja wetu,” amesema Namala.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here