Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
MKURUGENZI wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Dk. Suleiman Missango amesema kuwa Riba ya Benki Kuu (CRB) hutolewa kama Riba elekezi kwa mabenki kuweza kukopa fedha kutoka Benki Kuu.
Pia amefafanua sababu ya ongezeko la Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia sita kuwa ni kudhibiti mfumuko wa bei siku za usoni.
Hayo ameyabainisha Leo prili 8 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na waandishi wa habari wa vyombo tofauti Dk. Missango ili kutoa elimu kuhusiana na mfumo mpya wa sera ya fedha unatumia Riba ya Benki Kuu (CRB).
Amesema Benki Kuu imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mabenki ili kudhibiti ujazi wa fedha katika mabenki nkwenye mzunguko.
“Mfumo wa sera ya fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu utasaidia mabenki na taasisi nyingine za fedha kupanga viwango vyao vya Riba na sio kuweka ukomo wa riba kwa mabenki na taasisi zinazotoa mkopo,”amesema Dk. Missango.
Amesema mwenendo wa uchumi wa dunia ulikuwa unaashiria uwepo wa mfumuko wa bei hivyo ikaona iongeze riba kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia sita katika robo ya pili kuanzia Aprili mwaka huu.
Amesema kupanda kwa riba hiyo kumezingatia ukuaji wa uchumi kwa maana ya uwepo wa fedha za kutosha katika mzunguko kulingana na malengo yaliyowekwa.
“Wengi walijua tunakwenda kuweka ukomo wa riba sio kweli, kwa kupandisha riba hiyo maana yake tunapunguza ukwasi katika mzunguko na hivyo kudhibiti mfumuko wa bei kwa siku zijazo.
“Kupanda kwa riba hiyo kumezingatia ukuaji wa uchumi , maamuzi mengine yatachukuliwa Julai mwanzoni na riba hii ni ya robo ya kwanza ya Aprili, mwaka huu na inaweza kupungua au kuongezeka kwa kadri ya uchambuzi utakavyokuwa,” amesema Dk.Missango
Ameongeza kuwa tangu Benki Kuu ianzishe mfumo wa riba ya Benki Kuu mwaka huu badala ya mfumo wa zamani wa ujazi wa fedha hali imeendelea kuwa tulivu na mapokeo yamekuwa mazuri kwa wadau.
Ameeleza kuwa hali hiyo imetokana na juhudu kubwa ya kutoa elimu kwa wadau katika sekta na imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa wanananchi kuweza kufanya uamuzi sahihi katika shughuli za kiuchumi.