Home KITAIFA KAKOSO:ONGEZENI KASI UJENZI WA BRT 3

KAKOSO:ONGEZENI KASI UJENZI WA BRT 3

Dar es Salaam

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezungumzia umuhimu wa Serikali kumsimamia kikamilifu mkandarasi SINOHYDRO Corporation Ltd anaejenga Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT3) ili ukamilike kwa wakati.

Akizungumza leo Machi, 17 2025 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Moshi Kakoso amesema mradi huo unaoanzia katikati ya jiji la Dar es salam hadi Gongolamboto km 23.3 ukikamilika utapunguza msongamano na kuchoche shughuli za kiuchumi.

” Serikali imewekeza fedha nyingi katika barabara za BRT zilizozunguka jiji la Dar es Salaam hivyo hakikisheni zinakamilika na tija inaonekana kwa kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufika katika maeneo yao ya kazi na biashara kwa wakati.

“Tumejiridhisha na kasi inayoenda lakini tuna mashaka muda uliopangwa kumalizika kwa mradi huu umebaki miezi minne hivyo fanyeni kazi usiku na mchana ili aweze kukabidhi mapema”, amesema Kakosa.

Mwenyekiti Kakoso ameshauri Serikali kuangali sanifu za miradi ya barabara za BRT ili ziwezeshi pindi magari yanapopata dharula.

“Tunashauri watalaamu kuangalia maeneo ambayo hayana ulazima kuweka kingo wazipunguze au kutoa kwaajili ya kujenga mazingira rafiki ambayo yatasaidia miundombinu hii kuwapa fursa nzuri wananchi wanufaike nayo”, amesisitiza Kakoso.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi wa BRT 3 umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.

Ametoa rai kwa wananchi wanaofanyabiashara wakati ujenzi wa mradi huo unaendelea kuacha mara moja kwani licha ya kukwamisha kazi pia ni hatari kwa maisha yao.

“Namwagiza Mkandarasi aongeze mafundi, vibarua ili kukamilisha mradi huu ifikapo mwezi Juni,”amesema Kasekenya.

Kwa Upande wake Meneja wa Mradi wa BRT3, Mhandisi Frank Mbilinyi amesema BRT kwa kushirikiana na Serikali za mitaa na ustawi wa jamii wanaendelea kuwapa elimu wananchi ili kuacha kuvamia maeneo ambayo ni ya barabara na ujenzi unaendelea.

Serikali inaendelea kujenga barabara za kupunguza msongamano jijini Dar es salaam ambapo awamu ya kwanza Kivukoni-Kimara- Magomeni -Moroccco km 20.9 na awamu ya pili Magomeni- Mbagala imekamilika.

Awamu ya tatu Posta-Gongolambotokm 23.3 na awamu ya nne katikati ya jiji – Tegeta km 29.13 ujenzi wake unaendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here