Morogoro
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezungumzia umuhimu wa Wizara ya Ujenzi kuwekeza kikamilifu katika Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), ili kuongeza idadi ya mafundi stadi na sanifu na hivyo kukuza sekta ya ujenzi nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso amesema hayo leo Machi, 12 2025 wakati kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la taaluma katika makao makuu ya Taasisi hiyo mjini Morogoro.
“Hongereni kwa hatua kubwa ya ujenzi mliofikia hakikisheni ujenzi unakamilika kwa wakati ili muongeze idadi ya wanafunzi na hivyo kukuza kada ya ufundi badala ya kila mtaalam kuwa Mhandisi,”amesisitiza Kakoso.
Amesema kuwa uwepo wa mafundi mchundo na sanifu wengi utachochea ajira na kukuza sekta ya ujenzi na tasnia ya ufundi kwa ujumla.

Mwenyekiti huyo amezungumzia umuhimu wa ICoT kuongeza idadi ya walimu, kuwapa mafunzo ya mara kwa mara na kujenga majengo ya kisasa katika campus ya Mbeya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhndisi Godfrey Kasekenya ameishukuru Kamati hiyo ya Bunge kwa ushauri inaoutoa kwa Serikali katika kukuza sekta ya ujenzi na kuahidi kuufanyia kazi ili kufikia malengo ya kukuza idadi ya mafundi sanifu nchini.
“Tutahakikisha jengo hili linakamilika mwaka huu na kukarabati mengine ili kukuza Taasisi hii ambayo ni ya mfano kwa nchi na kuitangaza ili vijana wengi wanufaike na fursa zilizopo”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi ICoT ni Taasisi ya mafunzo chini ya Wizara ya Ujenzi ikiwa ni muunganiko wa kilichokuwa Chuo cha Ujenzi Morogoro (MWTI) na iliyokuwa Taasisi ya Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi (ATTI) Mbeya ambapo kada za ufundi stadi, sanifu na uhandisi ujenzi, umeme, bomba na mitambo hufundishwa katika campus zake za Morogoro na Mbeya.