Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameongoza hafla ya Polisi Family Day mkoa wa Mara iliyoambatana na utoaji tuzo kwa askari na wadau kwa mchango wao wa ulinzi na usalama.

Hafla hiyo imefanyika lmachi mosi kwenye viwanja vya kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia( FFU) mkoani Mara Katika hafla hiyo askari waliofanya vizuri katika kutimiza majukumu yao ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao wamekabidhiwa tuzo na kiasi cha shilingi laki tano.
Licha ya tuzo na kiasi hicho cha fedha kwa askari wadau mbalimbali walioshirikiana na jeshi hilo mkoani Mara nao wametambuliwa kwa kupewa vyeti vya pongezi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Kanali Mtambi amewapongeza askari waliofanya vizuri na kuwataka kuendelea kuzingatia maadili na kufuata maelekezo ya kutimiza majukumu.

Amesema maadili kwa askari ni jambo muhimu na la msingi kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye jamii kuanzia raia na mali zao.
Kwa upande wa wadau amesema suala la usalama ni la kila mmoja hivyo wada wanapaswa kushirikiana na jeshi la polisi kwaajili ya usalama.
“Niwapongeze sana askari na wadau ambao mchango wenu umetambuliwa katika suala zima la ulinzi na usalama kwa raia na mali zao,”amesema.

Mmoja wa wadau waliotambuliwa mchango wao Anifa Majura maarufu kwa jina la “mama Fugo” amelishukuru jeshi la polisi kwa kutambua mchango wake na ushirikiano kwa jeshi la polisi.
Amesema kupitia huduma za chakula na mapambo amekuwa na ushirikiano mzuri na jeshi hilo kila anapo hitajika.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi wa polisi, wadau wa usalama,viongozi wa dini pamoja na familia za maafisa wa polisi na askari.