Home BURUDANI RAIS DK.MWINYI AFUNGUA TRACE AWARDS 2025

RAIS DK.MWINYI AFUNGUA TRACE AWARDS 2025

Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono wasanii kwani ni muhimu katika kukuza Utalii, Uwekezaji na Urithi wa Utamaduni miongoni mwa Jamii.

Rais Dk. Mwinyi amesema hayo leo Februari, 24 2025 alipolifungua Tamasha la Tuzo za Muziki la Trace Awards kwa mwaka 2025 linalofanyika Hoteli ya The Mora Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja .

Aidha, ameeleza kuwa sanaa ya muziki ina nguvu kubwa ya kuiunganisha jamii na nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi , uwekezaji na ubunifu pamoja na kuibua vipaji vya vijana katika sanaa.

Rais Dk.Mwinyi ametoa rai kwa waandaaji na washiriki wa Tamasha hilo mbali na kufurahia muziki bali pia litumike kujenga ushirikiano, umoja na mahusiano mazuri miongoni mwa wasanii.

Ameupongeza Uongozi wa Taasisi ya Trace Award kwa kuamua Tamasha hilo kufanyika Zanzibar kwa mara ya Kwanza kwani litaitangaza Zanzibar Kimataifa pamoja na uukuza utalii na kubainisha fursa za uwekezaji na utamaduni.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewapongeza wadau na wafadhili mbalimbali kwa kufanikisha kufanyika kwa Tamasha hilo na kuahidi kuwa Serikali kuendelea kuweka mazingira bora zaidi kwa wasanii na kazi za sanaa kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana, fursa za ajira na urithi wa utamaduni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here