▪️Asema ushiriki wa Rais Dkt. Samia kwenye tuzo hizo ni kielelezo cha namna anavyothamini na kuiishi Imani ya Dini ya Kiislam na uhifadhi wa Qur’aan
▪️Asema tuzo hizo zinaimarisha imani ya dini na uwezo kwa vijana.
Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kupata elimu hiyo na kuwaandaa kuwa watu wema.

Ametoa wito huo leo Februari 23, 2025 alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za Kuhifadhi Qurani Tukufu. yanayofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Jukumu la kuhakikisha maadili bora ni la kwetu sote, madhehebu ya dini yakiwa na mchango mkubwa,”amesema.
Aidha, Majaliwa amehimiza madhehebu yote ya dini kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na utulivu hasa katika kipindi cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu. “Amani na utulivu ni moja ya Tunu katika nchi yetu” amesisitiza Majaliwa.

Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Majaliwa amesema kuwa yanatoa nafasi ya kujenga maadili bora ikiwemo uaminifu, umakini, na kujitolea.
“Washiriki wanajifunza umoja, upendo na mshikamano na wengine kwa ufanisi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kuwa mashindano hayo yanahamasisha jamii ya Kiislamu duniani kote kuwa na utamaduni wa kujisomea na kuhifadhi Qur’aan Tukufu.

“Hii inachangia kuendeleza utamaduni wa kuheshimu dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii.
“Mashindano haya yanawawezesha vijana na watoto kuonesha uwezo wao katika usomaji na uhifadhi wa Qur’aan Tukufu. Hii ni fursa muhimu kwao kukuza kipaji, kujivunia mafanikio yao, na pia kujenga nidhamu na uwajibikaji,”amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaamini mashindano hayo yatasaidia kuleta maendeleo ya kiroho kwa vijana na kuhamasisha jamii kwa ujumla.
“Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya na taasisi mbalimbali katika kukuza na kuhamasisha shughuli za kidini,”amesema.