Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza Wafanyabiashara kujiandaa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kufanya Biashara kwa Uadilifu na kuwa na Huruma kwa Wananchi.
Alhaj Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo Februari, 7 2025 alipozungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Jibril Mkunazini alipojumuika katika Sala ya Ijumaa.
Alhaj Dkt, Mwinyi amesema kumekuwa na kawaida na tabia ya Baadhi ya Wafanyabiashara kupandisha bei Bidhaa wakati huo.
Amefahamisha Kuwa Serikali imekuwa ikipunguza Ushuru katika Mwezi wa Ramadhani hivyo si jambo jema kwao kupandisha bei za bidhaa na kuwaongezea mzigo Wananchi.
“Hakikisheni Hampandishi bei za bidhaa kwani Mnawapa mzigo mzito Wananchi wa kutomudu kununua bidhaa hizo muhimu,” amesema.
Akizungumzia suala la Uchaguzi Mkuu Ujao Alhaj Dk. Mwinyi amewasisitiza Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi Kudumisha Amani ili Uchaguzi huo Ufanyike kwa Utulivu na Amani.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar Alhaj Dk. Mwinyi amefika Jamati la Jumuiya ya Ismailia Aga Khan Kiponda na Kusaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Kiongozi wa Jumuiya hiyo Aga Khan wa Nne Prince Shah Karim Al- Husseini aliyefariki hivi karibuni Mjini Lisbon Ureno akiwa na Miaka 88.