Home KITAIFA UCHAMBUZI WA MIFUMO WABAINI TAASISI ,OFISI NA IDARA KUNA UPOTEVU NA UFUJAJI...

UCHAMBUZI WA MIFUMO WABAINI TAASISI ,OFISI NA IDARA KUNA UPOTEVU NA UFUJAJI WA FEDHA ZA UMMA

Dar es salaam

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kinondoni imesema katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2024 wamefanya uchambuzi wa mifumo na wamebaini mianya ya rushwa katika maeneo ya Ofisi,Taasisi, na Idara kuna upotevu na ufujaji wa fedha za umma na baadhi ya wananchi kuonewa kutokana na kutokuwa na elimu juu ya mifumo iliyopo.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 6 ,2024 jijini Dar es salaam Mkuu wa TAKUKURU Kinondoni, Christian Nyakizee amebainisha kuwa wamefanya uchambuzi mifumo wa usimamizi na ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki( POS) katika Manispaa na kubaini baadhi ya watumishi kutowasilisha fedha za makusanyo katika akaunti ya serikali.

Amesema wahasibu wa Halmashauri kutofanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wakusanyaji wa ushauru na wakati mwingine ukaguzi kufanyika baada ya muda mrefu hivyo kusababisha mapato kupotea na fedha kufujwa.

“Tumebaini Watumishi kutowasilisha fedha za makusanyo hawachukuliwi hatua stahiki pale wanapobainika na wasio waaminifu ambao tulibaini wanagushi stakabadhi kwa kuandika kiasi kidogo kuliko kiasi halisi walichopokea kutoka kwa wateja,” amesema Nyakizee.

Ameeleza kuwa TAKUKURU iliendelea na uchambuzi wa mifumo na katika usomaji wa mita za Ankara za maji Dawasa Wilaya ya Ubungo na walibaini taarifa za malalamiko kutoka kwa wateja na zinapopokelewa zinachukua muda mrefu kushughulikiwa na baadhi ya mita ni chakavu hutoa taarifa zisizo sahihi nyingine zimesimama hazisomi huku nyingine zikiwa na ukungu hivyo hazisomeka vizuri na kupelekea msoma mita kusoma pasipokuwa na uhakika .

Nyakizee amebainisha kuwa walifanya Uchambuzi wa mfumo wa uondoshaji taka ngumu ngazi ya Kaya maeneo ya biashara katika Manispaa ya Kinondoni na walibaini Vyombo vya kukusanyia taka maeneo mengi ya Halmashauri hiyo havitoshelezi na idadi kubwa ya kaya hawahifadhi taka kwenye makasha wanahifadhi kwenye viroba na hawana elimu kabisa ya utenganishaji wa taka laini na taka ngumu.

Katika hatua nyingine taasisi hiyo katika kipindi wamefanikiwa kufuatilia miradi yenye thamani ya shilingi bilioni mbili iliyohusu sekta ya elimu na kukuta mapungufu ikiwemo kubadilishwa kibali cha awali.

Nyakizee amesema walifuatilia miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya bilioni mbili katika ya miradi hiyo miwili ni yenye thamani ya shilingi 144,8000,000 imekutwa na mapungufu madogo madogo na wahusika walishauriwa kurekebisha mapungufu hayo.

“Katika mradi mmoja wa ujenzi wenye thamani ya Tsh 90,000,000 ulibainika kubadilishwa kibali ikwani kibali cha awal kilichotolewa kilikuwa ni cha kufanya ukarabati wa majengo madarasa badala yake wakaanzisha Ujenzi upya ambapo kufanya hivyo ni kosa kisheria kubadili matumizi ya fedha bila kibali kutoka sehemu husika hivyo ofisi inaendelea na ufutiliaji wa kina wa suala hili,” amesema Nyakizee.

Hata hivyo walipokea malalamiko 85 na kati ya hayo malalamiko 46 yalihusu rushwa na 39 hayakuhusu rushwa na walalamikaji wengine wamewashauri wakafungue majalada na wengine wapeleke malalamiko yao sehemu sahihi yakashughulikiwe katika hatua mbalimbali.

Pia katika kipindi husika TAKUKURU Kinondoni wamefungua mashauri sita Mahakama ya Halmashauri ya Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo na Jamuhuri imeshinda mashauri mawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here