Home KITAIFA DK. MPANGO ASHIRIKI IBADA YA KUAGA MWILI WA MAMA MZAZI WA WAZIRI...

DK. MPANGO ASHIRIKI IBADA YA KUAGA MWILI WA MAMA MZAZI WA WAZIRI MKENDA

Kilimanjaro

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango leo Februari,6 2025, wameungana na viongozi na wananchi mbalimbali katika Ibada ya kumuaga marehemu Sekunda Massawe ambaye ni Mama mzazi wa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Pius X – Tarakea mkoani Kilimanjaro.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amesema Serikali, inashukuru kwa maisha ya mama Sekunda ambaye alimzaa na kumlea Profesa Mkenda ambaye amekuwa Mtendaji na Kiongozi mahiri katika utumishi wa umma, tangu alipokuwa anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam na katika nafasi mbalimbali alizoshika Serikalini.

Amesema Taifa linaendelea kufaidi matunda ya malezi bora na uchapakazi, ambayo mama Sekunda aliwapatia watoto wake.

Ametoa rai kwa wazazi na walezi kufanya kila jitihada kusomesha watoto, kuwafundisha maadili mema, kushika dini yao kiadilifu, na kufanya kazi kwa bidii kwa faida yao wenyewe, familia na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amesema kila mmoja anapaswa kujitahidi kuishi vema na binadamu wenzake na kufanya kazi kwa bidii katika nafasi mbalimbali ili kutoa mchango mzuri kwa familia na Taifa, na kuacha historia nzuri na mifano bora ya kuigwa na jamii.

Ameongeza kwamba ni muhimu kujiandaa kumrudia Muumba maana hakuna ajuaye siku wala saa.

Ibada ya kumuaga marehemu Sekunda Massawe imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi Mhashamu Ludovick Minde na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Viongozi wa Dini  pamoja na wananchi mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here