Dar es Salaam
KLABU ya Yanga Wana Jangnwani usiku huu wa saa Nne kamili, 4 Februari, 2025 wametoa taarifa rasmi kwa Umma juu ya kuvunja benchi la Ufundi lililokuwa chini ya Kocha wake, Raia wa Ujerumani, Seak Ramovic pamoja na msaidizi wake.
Katika hatua nyingine, wamemtangaza Kocha Mloud Hamd ambaye atashika mikoba ya Wana Jangwani hao kuanzia sasa.
Awali, jioni ya leo ziliibuka taarifa kuwa Kocha Ramovic ameagana na wachezaji juu ya kuondoka kwake ndani ya Kikosi hicho kinachofanya mazoezi yake Avic Town, Kigamboni Dar es salaam.
Aidha, Yanga wanatarajia kushuka dimbani kucheza mchezo wa ligi kuu NBC, Jumatano 5 Februari, 2025 dhidi ya KenGold utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Hata hivyo Lajiji Digital imeshuhudia maoni tofauti ya mashabiki na wadau wa Klabu hiyo ya Yanga juu ya maamuzi ya pande mbili ya Kocha na Klabu, ambapo baadhi wameonesha wasiwasi wao dhidi ya mbio za ubingwa wakiwahofia Watani zao wa jadi Simba SC, kwa namna ya mwendo wa Ligi kuu ya NBC ambapo kwa sasa timu hizo zimeachana kwa pointi moja.
Wengi wa mashabiki hao wameonesha wasiwasi wao kwa kutoa maoni katika kurasa rasmi Klabu kupitia Mtandao wa Instagram ikiwemo kuonesha kutokubalina na maamuzi hayo.