Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Mahakama ya Tanzania itakuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo kama yatakayobainishwa kwenye Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Rais Dk. Samia ameyasema hayo leo Februari, 3 2025 jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Sheria nchini na uzinduzi rasmi wa Shughuli za Mahakama kwa mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali yakiwa na kaulimbiu “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo”.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa Dira utavutia mitaji ya uwekezaji jambo litakalohitaji kuingia mikataba mbalimbali baina ya Serikali na sekta binafsi. Hivyo, ametoa rai kwa sekta zote zinazohusika na Haki Madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki.
Amefafanua katika miaka ijayo Tanzania inatarajia kuhushuhudia ongezeko kubwa la shughuli za kibiashara na kiuchumi, hali itakayoongeza uhitaji wa huduma za utoaji haki zinazohusiana na biashara hizo.
Kwa msingi huo, Rais Dk. Samia ameitaka Mahakama ya Tanzania na Mabaraza ya Mashauri ya Kodi kuwa wawezeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutenda haki kwa usawa na kwa wakati.
Vilevile, amempongeza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma na mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika utekelezaji wa huduma za sheria, ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA na msisitizo wa kisera unaowekwa na Mahakama katika kuimarisha.