Home AFYA WAGONJWA 12 KUFANYIWA UPASUAJI WA MGONGO KWA KUTUMIA MATUNDU MADOGO WAKATI WA...

WAGONJWA 12 KUFANYIWA UPASUAJI WA MGONGO KWA KUTUMIA MATUNDU MADOGO WAKATI WA KAMBI MAALUM YA MATIBABU MOI

Dar es Salaam

WAGONJWA 12 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mgongo kwa kutumia teknolojia mpya ya upasuaji kwa matundu madogo (Spine Endoscope) katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wakati wa kambi maalum ya mafunzo ya matibabu hayo yanayoendelea MOI.

Hayo yamebainishwa leo Februari 3, 2025 jijini Dar es Salaam Mratibu mwenza wa mafunzo hayo ambaye pia ni daktari bingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wa MOI, Dk. Hamis Shabani ambapo amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo madaktari wazawa kufanya upasuaji kwa teknlojia hiyo ya kisasa.

Dk. Shabani amesema kuwa baada ya kukamilika kwa hatua ya mafunzo kwa nadharia, Februari 5, 2025 wataanza kufanya upasauji wa mgongo kwa njia ya matundu madogo chini ya wakufunzi kutoka Chuo Kikuu ya Weill Cornell cha nchini Marekani ambapo wagonjwa 12 wanatarijiwa kufanyiwa upasuaji huo.

Akizungumza na wakufunzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amekishukuru Chuo Kikuu cha Weill Cornell kwa ushirikiano na amewaasa washiriki wa mafunzo hayo, kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuleta nafuu haraka kwa wagonjwa.

“Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtatumia skills (ujuzi) kufanya kwa vitendo upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu madogo, nimeambiwa kuwa sio mara yenu ya kwanza kuja katika Taasisi yetu (MOI) na hivyo natarajia haitokuwa mwisho kuja hapa na kutufundisha ujuzi mpya” amesema Dk. Mpoki na kuongeza

“Teknolojia hii itakuwa mwarobaini wa kupunguza siku za wagonjwa kukaa wodini muda mrefu baada ya kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo, ni huduma mpya inayoendana na mahitaji ya teknolojia ya sasa”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Mgongo kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell Medicine cha nchini Marekani, Profesa Osama Nezar Kashlan ameushukuru uongozi wa MOI kwa mapokezi yao na kusema kwamba wanajihisi wapo nyumbani na kuahidi ushrikiano kati ya MOI na chuo hicho utaendelea kudumishwa.

Mafunzo hayo yameanza leo Februari 3, 2025 na yatafikia tamati Ijumaa Februari 7, 2025, yameandaliwa na kuratibiwa na MOI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Weill Cornell Medicine cha nchini Marekani na kujumuisha washiriki kutoka Nigeria, Uganda, Ujerumani na Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here