Home UCHUMI GAVANA TUTUBA : WAFANYABIASHARA NA WANANCHI WANAOPATA FURSA YA MIKOPO YA SERIKALI...

GAVANA TUTUBA : WAFANYABIASHARA NA WANANCHI WANAOPATA FURSA YA MIKOPO YA SERIKALI WAREJESHE KWA WAKATI

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emanuel Tutuba ametoa wito kwa Wafanyabiashara na wananchi nchini wanaopata fursa ya mikopo ya serikali warejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kukopa.

Wito huo ameutoa leo Januari 31, 2025 jijini Dar es Salaam na Gavana Tutuba wakati wa kikao kilichowakutanisha BoT, Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Kampuni ya Airpay Tanzania, wadau kutoka Taasisi za kibenki na mitandao ya simu.

“Tumekutana leo kwasababu katika mikopo wanayotoa ZEEA kumekuwa na changamoto ya mikopo chechefu yaani kiwango kikubwa cha wasiorejesha mikopo hiyo. Sasa tumekutana kwa majadiliano lakini wao wenyewe wametengeneza utaratibu wa kidijitali ambao utawezesha watu wapewe mikopo kwa njia za kidigitali ili kurahisisha namna ya upataji wa mikopo pamoja na usimamizi na urejeshaji.

“Kwahiyo tunaendelea kuwahimiza wananchi kuwa mtu anapokuwa amekopa hizi fedha za serikali iwe ni rahisi na salama kuzirejesha kwa namna itakayofaa hapa tunapanua wigo wa matumizi ya mifumo ya kidigitali ili irahisishe urejeshaji wa haraka,” amesema.

Amesema kuwa, fedha ambazo hutolewa kwaajili ya kukopeshana lazima wakopaji warejeshe marejesho yao kwa muda waliopangiwa ili na wengine waweze kukopa.

“Unapochelewa kurejesha hizi fedha za serikali maana yake kwamba unawapunguzia wengine fursa ya kukopa, lakini kufanya hivyo inakuwa ni tabia mbaya kwani pamoja na kuwanyima wengine fursa pia mnaanza kutengeneza mazingira ya kuongeza viwango vya riba kwasababu serikali au benki inapokukopesha lazima ihakikishe kuwa inarejesha,” amesema Tutuba.

Amebainisha kuwa wao kama wasimamizi wa sekta wataendelea kuweka mifumo mizuri ya kuhakikisha kwamba serikali inawawezesha wananchi, na wale wananchi wanapata faida ili warejeshe na kuweza kuendelea na biashara zao.

Gavana Tutuba ameipongeza Kampuni ya Airpay kwa kuandaa mfumo huo wa kidijitali utakaorahisha utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohammed, amesema lengo la kikao hicho ni kujadiliana namna ya utoaji wa mikopo na urejeshaji hususani katika matumizi ya mfumo wa kidigitali.

Amefafanua kuwa, hadi kufikia Disemba mwaka jana wameshatoa mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 34.9 ikiwafikia wanufaika 23,969 ambapo wanawake ni 14,000 na wanaume 9,000.

“Lengo ni kuhakikisha sisi kama ZEEA tunapotoa mikopo yetu iwe kidigitali lakini kwenda pamoja na wenzetu wa mabenki pamoja na mitandao ya simu,” amesema Mohammed.

Pia Juma amesema anaishukuru kampuni ya Airtel na Benki ya TCB kuwa kampuni za kwanza za kifedha kuweza kukamilisha muunganisho wa mifumo ya malipo kidijitali na ZEEA pamoja na Airpay.

“Hichi kilichofanywa na kampuni hizi mbili kimesaidia na kimeonesha jinsi gani wanaunga mkono serikali katika kuhakikisha tunakuwa na uchumi jumuishi visiwani Zanzibar,”amesema.

Kwa upande wake Makamu wa Rais na Meneja Mikakati Kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore amesema lengo la Airpay kutengeneza mfumo huo ni kusaidia katika kuweka uwazi na kurahisisha kulipa mkopo kwa wakati.

“Changamoto inapatikana ni pale mteja anapotaka kulipa mkopo wake, kwahiyo sisi tumerahisisha kwamba mteja anaweza kwenda kwa wakala na kulipa mkopo wake. Hii mifumo iko tayari, changamoto tunayoiangalia ni pale mteja ameshindwa kulipa au ameamua kutokulipa.

“Hii ni changamoto kwa serikali, ule mkopo unakuwa chechefu, kwahiyo leo tumekuja kuomba BoT ituruhusu kuchukua asilimia 33 ya kile ambacho kipo kwenye simu yake ili aweze kulipa kidogo kidogo…Hiyo inatokana na kwamba tayari mteja tumeshamtafuta na kumpigia simu lakini amekimbia, tunataka tutengeneze tabia ya urejeshaji wa mikopo, sio kwamba asilimia kubwa ya watanzania hawataki kulipa mkopo ila ile asilimia ndogo itachafua wale wengine,” amesema Wilmore.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here