Home KITAIFA RAIS DK.SAMIA : HAJAWAHI KUTOA MAELEKEZO KWA MTU YEYOTE ASILIPE KODI

RAIS DK.SAMIA : HAJAWAHI KUTOA MAELEKEZO KWA MTU YEYOTE ASILIPE KODI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amesema hajawahi kutoa maelekezo kwa mtu yeyote asilipe kodi na kusisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili kujenga maendeleo ya nchi.

DK.Samia ametoa kauli hiyo Januari, 23 2025 usiku wakati wa hafla ya tuzo za mlipa kodi zilizoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema wapo watu ambao wanatumia mwanya wa majina ya viongozi kukwepa kodi kwa maelezo kuwa anafanya hivyo kwa maelekezo kutoka juu.

“Katika nchi hii mtu wa ni rais ndiye anayepaswa kutoa maelekezo kutoka juu,hakuna aliye juu zaidi yangu,mtu akisema ameagizwa kutoka juu na kutoa maelezo hapaswi kulipa anamaanisha ni raisi,mimi sijawahi kufanya hivyo.

“Sijawahi kutoa maelekezo mtu asilipe kodi,endapo ikitokea haja ama ulazima wa kufanya hivyo nitatoa kwa maandishi,”amesema Dk.Samia.

Akizungumzia kuhusu walipa kodi ambao ni wafanyabiashara na wameshinda tuzo Rais Dk.Samia alisema serikali inathamini mchango wa wafanyabiashara wanaolipa kodi ambazo zinasaidia kuleta maendeleo.

“Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri zaidi wafanyabiashara ili kukuza ajira kwa wananchi pamoja na mapato ya serikali,tunataka kuwa na mfumo wa kodi utakaorahisisha kukua na kuchagiza uchumi,”amesema Dk.Samia.

Amesema serikali kupitia TRA inatumia fedha nyingi kujenga mifumo ya Tehama hivyo inapaswa kuwa na faida na isomana
ili wafanyabiashara walipe kodi masaa 24.

Rais Samia ameitaka TRA kuendelea kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa kuwasaka wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia Stempu bandia kwenye vinywaji.

“Dhuruma siyo kitu kizuri hivyo wanaokwepa Kodi watambue kuwa wanafanya dhuruma Hali kadhalika watumishi wa TRA wanaofanya makadirio yasiyokuwa sahihi nao wanafanya dhuruma, tuache,” Dk. Samia.

Dk. Samia amesema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza idadi ya Walipakodi na siyo kuwatumia wachache waliopo na Hali hii itafanikishwa na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi na kulipa Kodi kikamilifu.

Rais Samia amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaitaka Nchi ipunguze utegemezi na utegemezi huo utapungua kwa kusimamia kwa usahihi ukusanyaji wa Kodi jambo ambalo litaifanya Tanzania ijiamini.

Rais Samia amesema Bajeti ya Serikali ni shilingi Trilion 49.34 na miongoni mwa fedha hizo shilingi Trilion 30.4 sawa na asilimia 61.6 inatokana na makusanyo ya Kodi kutoka kwa TRA hiyo ndiyo inaonyesha tunavyouendea kujitegemea hivyo ongezeni juhudi katika kukusanya kodi.

Kuhusu masuala ya kesi za kikodi ameitaka Bodi ya rufani kuharakisha usikilizaji wa kesi hizo ili Kila mmoja apate haki yake.

Naye Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba akiwa katika utoaji wa tuzo za Mlipakodi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa miongozo anayoitoa katika ukusanyaji wa Kodi bila kutumia mabavu.

Amesema kauli ya Rais kutaka Kodi ikusanywe kwa hiari imezaa matunda kwa kupatikana kwa makusanyo makubwa ya Kodi pia Mhe. Rais ameunda Tume ya kufanya mapitio ya Sheria za Kodi na pia kuiwezesha TRA kujenga mifumo inayoweza kuleta tija kwenye makusanyo.

Dk. Mwigulu amesema katika kipindi hiki cha Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kwa kiasi kikubwa fedha katika sekta ya Kilimo, huduma za jamii, sekta ya Afya na katika Miundombinu ambapo barabara zinajengwa mijini na vijijini.

Swali Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda akiwa katika maadhimisho ya siku ya Mlipakodi Jijini Dar es Salaam amesema siku ya Shukrani kwa Mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua na kuwashukuru Walipakodi wote wakubwa na wadogo.

Amesema utoaji wa tuzo ni kutambua Walipakodi waliyofanya vizuri katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya Madini, Taasisi za Umma, Taasisi za Fedha, Sekta ya uzalishaji na Viwanda, Sekta ya Utalii, Walipakodi wakubwa na Tuzo ya Kamishna Mkuu.

Kamishna Mkuu Mwenda amevitaja vigezo vitano vilivyotumika kuwapata washindi wa tuzo kuwa ni Mlipakodi mwenye rekodi nzuri katika ulipaji wa Kodi, Mlipakodi anayelipa kwa hiari na kwa wakati, Mlipakodi anayetumia EFD mashine na VFD kikamilifu, Mlipakodi aliyelipa kodi kubwa zaidi na Mlipakodi anayetoa ushirikiano kwa TRA.

Amesema wapo washindi waliofanikisha makusanyo makubwa ya Kodi katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo TRA ilivuka malengo kwa kukusanya Sh. Trilion 16.528 ambao pia watatunukiwa.

“Mimi na wenzangu ndani ya TRA Tutaendelea kutekeleza maagizo yako yote, Tutaendelea kupambana na wanaofanya magendo, Tutaendelea kukusanya Kodi kwa kiwango kikubwa bila kuwa na migongano na Walipakodi, Tutaendelea kutatua migogoro na kuwasikiliza Walipakodi, Tutaendelea kutoa huduma Bora,” Kamishna Mkuu Mwenda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here