Home KITAIFA UJENZI WA RELI YA KISASA (SGR) KIGOMA HADI BUJUMBURA KUTUMIKA TIRIONI 6.3

UJENZI WA RELI YA KISASA (SGR) KIGOMA HADI BUJUMBURA KUTUMIKA TIRIONI 6.3

Kigoma

WAZIRI wa Uchukuzi Profesa, Makame Mbarawa amesema serikali ya Tanzania hivi karibuni inatarajia kuingia mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Bujumbura nchini Burundi ambapo badaye reli hiyo inatarajiwa kuendelezwa kujengwa kutoka Bujumbura hadi Kindu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Profesa Mbarawa ameyasema Januari, 23 2025 alipotembelea kipande cha sita cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tabora hadi kigoma yenye urefu wa kilometa 506 mradi unaogharimu kiasi cha shilingi trilioni 6.3 huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika Machi 2027.

“Wale wanaosema Kigoma ni mwisho wa reli, miaka miwili au mitatu ijayo hilo jambo litabadirika na Kigoma sasa itakuwa ni katikati ya reli,” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha kuhusu ujenzi wa SGR kipande hicho cha sita Waziri Profesa Mbarawa amesema kuwa kumekuwepo changamoto mbalimbali ambazo mkandarasi amezieleza lakini waatalamu wapo na wanazifanyia kazi changamoto hizo ambazo nyingi ni za kihandisi na kuwahakikishia wananchi kuwa kazi hiyo itakwenda kwa kasi inayotakiwa.

Meneja wa mradi huo, Mhandisi Wallace Isaya amesema kuwa ujenzi huo umekuwa na changamoto katika eneo la mto Maragarasi kutokana na mvua nyingi ambazo huathiri eneo hilo kwa kipindi cha takribani miezi saba kila mwaka na kubainisha kuwa hata hivyo katika msimu wa kiangazi uliopita mkandarasi amefanikiwa kujenga nguzo 13 za daraja hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani amesema kuwa Kigoma ilikuwa inaonekana iko mbali lakini kwa miradi kama hiyo haitakuwa mbali tena kwani wananchi wataweza kusafiri kwa urahisi mara itakapokuwa imekamilika.

Pia Mathamani ameishukuru serikali kwa uwekezaji huo na kuufungua mkoa wa Kigoma huku akibainisha kuwa miradi hiyo italeta fursa za kiuchumi kwa wananchi kwani wawekezaji wengi watafika mkoani humo kutokana na ardhi yao kuwa ni yenye rutuba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here