Home KITAIFA NECTA YAWAFUTIA MATOKEO WATAHINIWA 67 KWA UDANGANYIFU

NECTA YAWAFUTIA MATOKEO WATAHINIWA 67 KWA UDANGANYIFU

Dar es Salaam

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limewafutia matokeo watahiniwa 67 waliofanya udanganyifu wakati wa mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka 2024.

Akitangaza matokeo hayo leo, Januari, 25 2025 jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa NECTA,Dk. Said Mohamed amesema katika idadi hiyo wapo wanafunzi watano walioandika lugha ya matusi katika karatasi zao za mtihani wa kidato cha nne.

“Matokeo haya yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani mwaka 2016,” amesema Dk. Mohamed.

Amesema NECTA limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 459 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani wa kidato cha nne 2024 kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

Amesema watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha Kanuni za mtihani.

Pia NECTA imekifungia kituo cha p6384 BSL Open School kilichopo mkoa wa Shinyanga kuwa kituo cha mitihani ya Taifa kutokana mipango ya udanganyifu.

“Kituo hiki kimefungwa kwa mujibu wa kifungu 4 (8) cha kanuni za mtihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa Mitihani ya Taifa,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ubora wa ufaulu Dk. Mohamed alisema watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja ya l-lll kwa mwaka 2024 ni 221,953 sawa na asilimia 42.96.

Amesema mwaka 2023 watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja I-III walikuwa 197,426 sawa na asilimia 37.42 hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 5.54 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Dk. Mohamed ameeleza kuwa ubora wa ufaulu wa madaraja I-III ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na wasichana ambapo wavulana ni 119, 869 sawa na asilimia 48.90 ya wavulana wote wenye matokeo na wasichana ni 102, 084 sawa na asilimia 37.59 .

Dk. Mohamed ametoa tathimini ya jumla ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2024 alisema Jumla ya ya watahiniwa 557, 796 waliosajiliwa kufanya mtihani huo amapo wasichana 296, 051 sawa na asilimia 53.08 na wavulana 261,745 sawa na asilimia 46.92.

Amesema kati ya watahiniwa 557,796 waliosajiliwa watahiniwa wa shule walikuwa 529,329 na watahiniwa wakujitegemea walikuwa 28,467.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here