Dar es Salaam
WATUMISHI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kuzingatia kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwa lengo la kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa ustawi wa wananchi katika sekta ya afya.
Hayo yamebainishwa leo Januari 21, 2025 na Afisa Habari Mkuu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Rocky Setembo, wakati akiwasilisha mada ya kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma.
Setembo amesema kuwa ni vema watumishi hao kuzingatia kanuni za utendaji ya maadili katika utumishi wa umma kwa kujua sera, miongozo, kanuni, taratibu na sheria zilizoanzisha taasisi zao ili waweze kuboresha ustawi wa wananchi katika sehemu za kazi.
“Kila taasisi mnayoijua imeanzishwa kwa sheria fulani, kwahiyo taasisi ikishaanzishwa na yenyewe inatengeneza miongozo, sera na taratibu za kuzifuata ili kuweza kutekeleza majukumu yake, hiyo itasaidia kutoa huduma bora kwa viwango vya juu na kuleta ustawi wa wananchi,” amesema Setembo.
Aidha, Setembo amezitaja baadhi ya kanuni za maadili katika utumishi wa umma kuwa ni kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uaminifu, Kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya taarifa.
Pamoja na mambo mengine, Setembo amewaasa watumishi hao kuepuka matumizi ya pombe kupindukia na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile bangi, mirungi.
Naye, mkurugenzi msaidizi, idara ya usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma, Ally Ngowo amesema kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kila mwaka huandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuwakumbusha watumishi maadili ya utendaji katika utumishi wa umma ili watumishi hao waweze kujua haki na wajibu wao katika kutetekeleza majukumu yao ya kila siku.