Dar es Salaam
MABORESHO yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kwenye upande wakupokea na kupakua mizigo yamesababisha kupunguza siku za wafanyabiashara kupokea mizigo baada ya meli kuwasili kutoka kumi mpaka tatu huku ikiwataka wafanyabiashara kufuata mizigo yao kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari, 15 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari hiyo, Abeid Galusi wakati wa ziara ya viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) ambao walitembelea katika bandari ya Dar es Salaam.
Amesema mabadiliko hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa na kampuni mbili DP World na Aidan ports na kusisitiza kuwa kwa sasa kumekuwa na mlundikano wa mizigo kutokana na wafanyabiashara kutofuata mizigo yao kwa wakati.
“Ujio umeleta mabadiliko katika muda wa kusubiri mizigo kwenye meli umepungua kutoka siku kumi za awali hadi tatu kwa sasa,tunawaomba wateja wetu waje kuchukua mizigo kwa wakati kwakuwa sasa mizigo ipo mingi hivyo waongeze kasi ya kuichukua,”amesema Galusi.
Amesema uingizaji wa mizigo pia umeongezeka kwa asilimia 60 kwa nchi jirani huku kwa mizigo ya ndani imeongezeka kwa asilimia 40.
Amsema mizigo mingi ya nchi jirani inayoingia inaenda Congo, Zambia na Rwanda.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Nchini (JWT), Hamisi Livembe amesema uwekezaji wa bandari umeboresha utoaji wa huduma katika bandari na kuondoa malalamiko yaliyokuwepo Kwa wafanyabiashara.
Ameeleza kuwa ujio wa Dp World na Adani Ports katika kuendesha shughuli za bandari imerahisisha ushushwaji wa mizigo na kuchukua muda mfupi tofauti na awali ambapo kulikuwa na ucheleweshaji.
“Mwaka juzi kulikuwa na malalamiko ucheleweshaji mizigo meli ilikuwa inakaa siku 30 hadi 40,kuna kipindi mzigo ulikuwa unakaa ushuru unafika hadi Dola 8000 sababu ya ucheleweshaji,”amesema.
Amesema kwa sasa meli hazikai lakini pia meli zinatoka haraka tunasikia kutoka kwa wafanyabiashata na sisi ni mashuhuda.
“Mabadiliko ni makubwa na bado wanaendelea na uwekezaji,tumeona mashine mbili ambazo zinashusha kontena 1000 kwa siku na bado wanataka kuongeza mashine nyingine,mafanikio ni makubwa tunawapongeza TPA na serikali Kwa jitihada hizi,”amesema.
Kwa upande wa Meneja wa Uhusiano wa kampuni ya DP World, Elitunu Mallamia amesema wamejitahidi kuongeza ufanisi na kuvunja rekodi Kwa mwezi Desemba wamehudumia meli 27 huku changamoto iliyopo sasa wateja kuondosha mizigo.
“Tunatoa Rai kwa wateja kuondosha mizigo yao mapema ili nasi tuongeze mizigo kwenye ICD kontena zaidi 220000 zimeingia kama bandari tumevuka malengo kwa kiwango kontena milioni moja kuyahudumia kwa mwaka,”amesema.