Home KITAIFA ERB ONGEZENI UBUNIFU KUENDANA NA SAYANSI NA TEKNOLOJIA – WAZIRIULEGA.

ERB ONGEZENI UBUNIFU KUENDANA NA SAYANSI NA TEKNOLOJIA – WAZIRIULEGA.

Morogoro

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), kuongeza ubunifu ili kuendana na kasi mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

Waziri Ulega amesema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa ERB mjini Morogoro leo Januari 13, 2025 ambapo amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Teknolojia katika uhandisi ili kuwa na miradi imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.

Aidha Waziri Ulega ametaka wahandisi wachanga kupata fursa nyingi katika ujenzi wa miradi mikubwa na ya kimkakati inayoendelea nchini ili waweze kupata ujuzi na uzoefu.

“Tija na ubunifu vitafikiwa kwa ERB kushirikiana kikamilifu na wadau wa kijamii, sekta binafsi na taasisi za elimu,”amesisitiza Ulega.

Ameipongeza ERB kwa kuanzisha program ya kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi, kuanzisha shule ya wahandisi na kuendelea kusajili na kusimamia mienendo na weledi wa wahandisi wote nchini.

” Hakikisheni mnakuwa na mfumo mzuri wa kuratibu, kutathmini na kufuatilia shughuli za kihandisi ili kuleta tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesisitiza Ulega.

Naibu Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi Dk. Charles Msonde amesema Wizara itaendelea kuiwezesha ERB ili ifanye kazi nyingi kuendeleza wahandisi kwa maslahi ya umma.

Naye Msajili wa ERB Mhandisi Bernard Kavishe amesema Bodi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1968 inaratibu taaluma na mienendo ya wahandisi na mafundi sanifu zaidi ya elfu 41 nchini.

“Tumejipanga kuhakikisha wahandisi na mafundi sanifu wanafanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kukidhi mahitaji ya wakati”, amesema Mhandisi Kavishe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Musa Kilakala amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miradi ya barabara ya Bigwa-Kisaki KM 78 na SGR -Kihonda na kusisitiza kukamilika kwa miradi hiyo kutakuza uchumi wa wananchi wa Morogoro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here