Home KITAIFA RAIS DK.MWINYI: AMEUAGIZA MFUKO WA BARABARA KUFANYIA UKARABATI BARABARA MPYA ZOTE

RAIS DK.MWINYI: AMEUAGIZA MFUKO WA BARABARA KUFANYIA UKARABATI BARABARA MPYA ZOTE

Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameuagiza Mfuko wa Barabara kuzifanyia ukarabati barabara mpya zote mara tuu zitakapopata hitilafu kwa kuzitengeneza na kuzipaka rangi ili kuzirejesha kwenye haiba yake.

Aidha, amezitaka mamlaka zinazosimamia hifadhi ya barabara kuendelea kuwaelimisha wananchi wasijenge karibu na hifadhi ili kuinusuru Serikali kubeba mzigo mkubwa wa kulipa fidia inapotaka kupitisha miundombinu ya jamii ikiwemo kuzitanua barabara hizo na kupitisha huduma nyengine za mawasiliano.

Akizungumza leo Disemba, 24 2024 kwenye hafla ya ufunguzi wa barabara ya kilomita 6.5 inayotoka Uwanja wa ndege, Wilaya ya Magharibi B hadi Mnazi Mmoja Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, iliyopewa jina la “Uwanja wa ndege – K/Samaki” Rais Dk. Mwinyi ameiasa jamii kutozitumia njia za wapita kwa miguu kinyume na makusudio yaliyowekwa na Serikali, kufanya hivyo ni kosa la matumizi ya barabara hizo.

Amesema ni kosa pia kwa wenye vyombo vya moto ikiwemo magari na vyombo vyengine kuzitumia barabara za watembea kwa miguu kwa maegesho ya vyombo vyao ama shughuli nyengine za kijamii, akiwatolea mfano wafanyabiasha waliopembezoni mwa barabara hizo na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema uzinduzi wa barabara hiyo ya Uwanja wa ndege – K/Samaki unakamilisha kilomita 109 za barabara zote za mjini ambazo Serikali iliahidi kuzijenga kwa sababu nyingi zilichakaa, sambamba na kujengwa Flyover awamu ya kwanza ya Mwanakwerekwe na ile nambari mbili ya Amani ambazo zitakamilishwa pia ujenzi wa makutano ya barabara nyengine zitakazobeba njia mbili za Kwenda na kurudi, (Interchange Road) ambazo zitaondosha foleni, msongamano na usumbufu kwa wananchi wakiwa kwenye harakati zao za kila siku.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi ameridhia maombi wa wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kuwekewa taa za barabani kwenye ujenzi wa barabara yao ya kwanza inayojengwa kisiwani humo kwa nguvu za Serikali.

Aidha, Dk. Mwinyi ameagiza barabara mpya zote na kila zitakazojengwa upya lazima ziwekwe taa za barabrani ili kung’arisha haiba ya mji kulikangana na ubora wa barabara hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here