Dar es SalaamÂ
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Majaji wanawake Tanzania (TAWJA) ambayo yatafanyika kwa siku tano kuanzia Januari 19-23, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha.
Akizungumza leo Disemba, 19 2024 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa rufani Barke Sehel amesema wamemuomba Rais kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.
Amesema siku hiyo masuala mbalimbali yatajadiliwa ikiwamo masuala ya haki na usawa wa kijinsia.
“Kwenye maadhimisho haya tutaeleza changamoto mablimbali ikiwamo hii ya ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti na nini kifanyike,” amesema.
Jaji Sehel aligusia pia ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti ambazo amesema kwa miaka ya hivi karibuni matukio ya ubakaji na ulawiti yameongezeka kwenye mikoa karibu yote.
“Miaka ya nyuma kesi za namna hii zilisikika kwenye baadhi ya mikoa, lakini miaka ya karibu mikoa yote inamatukio haya tena kwa kiwango cha juu.
“TAWJA tunafanya jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwenye masuala ya usawa wa kijinsia,”amesema.
Akizungumzia miaka 25 ya Chama hicho, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Taifa, Sophia Wambura amesema katika kipindi hicho TAWJA imefanikiwa kukuza hali ya usawa kwenye ngazi ya utendaji wa Mahakama.
“Vilevile tumehamasisha usawa kwenye jamii katika kuijengea uwezo kutambua haki zao katika mirathi, talaka na haki za usawa na masuala mengine ya kijamii,” amesema.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha na mwenyekiti wa kamati mwenyeji ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Aisha Bade amesema bado kuna changamoto za dhamana.
Amesema pamoja na kwamba dhamana zinakua wazi lakini wahusika wanashidwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kukosa baadhi ya mahitaji kama mdhamini na vitambulisho, jambo ambalo katika maadhimisho hayo pia watatoa elimu hiyo.
Maadhimisho hayo pia yatashirikisha wadau wengine ikiwamo majaji na mahakimu wanawake kutoka Bara na Zanzibar sambamba na washirika wa kimataifa kama UN Woman, UNDP na UNICEF.