Home KITAIFA WAZIRI ULEGA ATEMA CHECHE TANROADS

WAZIRI ULEGA ATEMA CHECHE TANROADS

Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura iliyo chini yake.

Waziri Ulega ametoa maagizo hayo Disemba,18 2024 kwenye mkutano wake na Menejimenti na Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini uliofanyika mjini Dodoma ambapo aliwaambia miradi ya dharura inapaswa kushughulikiwa kidharura.

“Fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususan kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa”, amesema Ulega.

Ulega amewaambia mameneja hao kuwa wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.

Ulega alisema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na zile za El Niño zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.

Mkutano wa Dodoma ulikuwa ni wa kwanza kwa Ulega kukutana na viongozi wa TANROADS tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais Samia Suluhu Hassan mwezi huu.

Waziri huyo mpya ametumia nafasi hiyo kupongeza wafanyakazi wa wakala hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imekamilisha ujenzi wa barabara zaidi ya Kilometa 1,198 kwa kiwango cha lami.

Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, amewataka mameneja hao kufanya kazi kwa kujiamini na weledi mkubwa ili kuleta tija na ufanisi katika Sekta ya Ujenzi nchini ili kuondoa kero ya miundombinu mibovu kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha, ametoa rai kwa Mameneja wa Mikoa yote nchini kuhakikisha maeneo yote yenye msongamamo wa magari hususani kwenye majiji na Manispaa yanafanyiwa usanifu yakinifu kwa ufasaha kulingana na mahitaji ya sasa na miaka mingi ijayo na kuratibiwa vizuri ili kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao kwa wakati.

Waziri Ulega amewahakikishia Mameneja hao kuwa Serikali awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Wakandarasi ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kasi ili kuendana na malengo ya Serikali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara kuu, za mikoa na madaraja yanajengwa ili kupitika wakati wote wa mwaka.

Balozi Aisha amewataka Mameneja wa TANROADS kuboresha usimamizi wa miradi, kulinda hifadhi za barabara pamoja na kupendezesha miji kwa taa za barabarani na utunzaji wa mazingira pembezoni mwa barabara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here