Home KIMATAIFA TANZAN IA NA OMANI ZASAINI MKATABA WA KUTOTOZA KODI MARA MBILI

TANZAN IA NA OMANI ZASAINI MKATABA WA KUTOTOZA KODI MARA MBILI

Na Benny Mwaipaja, Oman

SERIKALI yanJamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion.

Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut nchini Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi.
Dk. Nchemba amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika jitihada Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kufungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Ameongeza kuwa  Mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi wa biashara kwa pande zote mbili.
Mkataba huo pia unalenga kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hususan kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sambamba na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na kuongezeka kwa ajira kwa wananchi.
Aidha, wawekezaji wa Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili. 

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.
Kwa ujumla, Dk. Nchemba amesema kuwa mkataba huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi, na mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here