Dar es Salaam
WALINZI wanaotoa huduma Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamekumbushwa kuzingatia misingi ya utoaji huduma bora wanapotekeleza majukumu yao kwa wateja wa ndani na nje wanaokuja kupata huduma mbalimbali hospitalini hapo.
Hayo yameelezwa leo Disemba, 16 2024 Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambaye pia ni Muuguzi Mtalaam wa Afya ya Akili na Mkufunzi wa Mafunzo ya Utoaji Huduma Bora kwa Wateja, Sofia Sanga wakati akitoa mafunzo kwa walinzi wanaolinda maeneo mbalimbali ya hospitali.
Sanga amewakumbusha walinzi hao kuwajulia hali wanao wahudumia, kutokuwa na lugha ya ukali, kuonesha tabasamu wanapotoa huduma, kuwa wasikivu, kuwa wepesi kutoa huduma, kutoa huduma yenye usawa, kuelekeza kwa upendo, kuwafanya wateja wajione wa muhimu na wa thamani, kutambua wenye mahitaji maalum kwani huduma bora kwa mteja hukamilika pale tu anaporidhishwa na jinsi alivyohudumiwa.
Akifungua mafunzo hayo kwa kundi la kwanza la walinzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Aminiel Aligaesha, amesema walinzi ni kada muhimu katika taasisi kwani wao ndiyo wa kwanza kuwasiliana na wateja wanaofika hospitalini hapo ili kupata huduma hivyo wana mchango mkubwa katika hatua mbalimbali za utoaji huduma.
“Tunatoa mafunzo haya kwa kada hii ili waweze kufahamu matarajio yetu kwao, kwani ni wajibu wetu sisi watoa huduma za afya kutoa huduma bora kwa wananchi wanaotumia huduma zetu,” amesisitiza Aligaesha.
Kwa upande wa Walinzi wamekiri kuwa mafunzo hayo watayazingatia katika kutekeleza majukumu yao na kuongeza kuwa watajitahidi kuwaelekeza kwa weledi wateja ambao hawapendi kufuata utaratibu wa hospitali hususani kwenye maegesho ya gari, muda wa kuona wagonjwa wodini na taratibu nyingine za hospitali.