Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwenye kampeni ya kupima afya ya moyo bure kwa wasanii, inayotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 21, 2024, hadi Januari 2025. Kampeni hiyo itatoa fursa kwa wasanii wa filamu kupima afya zao na kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo.
Hayo ameyasema Disemba, 13 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo itakayotolewa kwa wasanii wote nchi nzima.
Amesema kutokana na tatizo la magonjwa ya moyo ni kubwa Taasisi hiyo imeona ishirikiane na wasanii katika kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kupima magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Katika kufanikisha hili kutakuwa na zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo kwa wasanii katika kliniki yetu ya Kawe kwa mwezi wa huu wa Desemba hadi Januari 2025 kila siku za Jumamosi na Jumapili.
“Baada ya kumalizika kwa zoezi hili kutakuwa na utaratibu maalumu kwa wasanii ambao hawana bima za afya watakaokuja kutibiwa katika kliniki ya moyo Kawe iliyopo health plaza watapata punguzo la gharama za matibabu,”amesema Dk. Kisenge.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na Mwanao, Steve Mengele maarufu kama “Steve Nyerere,” amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwapa wasanii wa filamu fursa ya kupima afya zao ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya moyo.
Aidha, amewasihi Watanzania wote kupima afya zao mara kwa mara ili kufahamu hali ya afya na kuishi maisha yenye umakini, kwa kuzingatia ulaji unaofaa.
“Wajitokeze kwa wingi kujisajili kwenye mamlaka zilizokasimiwa, ikiwemo Bodi ya Filamu Nchini pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA), kwa ajili ya kutambulika na kupata huduma ya kupima afya bila gharama yoyote,” amesema Steve Nyerere.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi hata katika maeneo ya pembezoni.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dk. Kedmon Mapana ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kupima a fya za mioyo ya wasanii na kuwapa elimu ya jinsi ya kujiepusha na magonjwa hayo bila ya gharama zozote zile.
“BASATA tutasimamia zoezi hili la upimaji kwa wasanii wetu ili kila mmoja anufaike na upimaji huu kama mlivyosikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo ni kubwa hivyo basi ni muhimu mkachukuwa hatua za kupima mapema kabla ya kusubiri kuugua”, amesisitiza Dk. Mapana.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dk. Gervas Kasiga amesema upimaji huo ni wa muhimu kwani utawapa hamasa wasanii ya kupima mioyo yao na kuchukuwa hatua baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo.
“Ninawasihi mtumie vizuri fursa hii kwa kupima mioyo yenu na kupata elimu ya jinsi ya kujiepuka na magonjwa haya pia elimu mtakayoipata muitumie kuielimisha jamii inayowazunguka kwani uwezo wa kufanya hivyo mnao,”amesema Dk. Gervas.