Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wito kwa wabunifu, wahandisi, na wadau wote wa Sekta ya Ujenzi kuhakikisha kila mradi wa ujenzi unazingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira, kupunguza taka zinazozalishwa na kuongeza ufanisi wa rasilimali.
Kasekenya ametoa wito huo katika hafla ya Tuzo za Ujenzi na Majengo ya Afrika Mashariki zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Mkoani Dar es Salaam Disemba,12 2024 na kubebwa na kauli mbiu “Embracing Digital Transformation in Construction” na kuangazia maendeleo ya Sekta ya Majengo kupitia teknolojia na ubunifu.
Kasekenya ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Sekta ya Ujenzi ili kuhakikisha Afrika Mashariki inakuwa kiongozi wa mabadiliko ya kidijitali kwa kutumia maarifa, teknolojia na uvumbuzi mbalimbali.
“Niwahakikishie kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa katika Sekta ya Ujenzi kupitia Sera na Programu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa dhana ya ujenzi endelevu inatekelezwa kikamilifu”, ameeleza Mhandisi Kasekenya.
Aidha, Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa katika nchi za Afrika Mashariki ni wakati muafaka wa kuwekeza katika miradi inayozingatia uendelevu na yenye athari ndogo kwa mazingira kwa kuhusisha matumizi ya vifaa vya kijani, nishati safi na ubunifu wa majengo yanayoweza kuhimili hali mbalimbali za hewa.
Amebainisha kuwa tuzo hizo za ujenzi na majengo za Afrika Mashariki zinalenga kuongeza ushindani miongoni mwa wadau wa Sekta ya Ujenzi pamoja na kuwa chachu ya utoaji wa huduma bora.
Vilevile, amewapongeza waandaaji wa tuzo hizo kwa juhudi zao katika kuleta pamoja wadau wa Sekta ya Ujenzi ili kutambua na kuhamasisha uvumbuzi na ufanisi katika sekta hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Chemba ya Sekta ya UjenziTanzania (CCIT), Pamela David Shoo amesema kuwa lengo la kuanzisha tuzo hizo ni kuwatambua watu binafsi na makampuni ambayo yametoa huduma bora za ujenzi kwa kipindi cha miezi 12.