Na Farida Ramadhani na Chedaiwe Msuya, Dar es salaamn
SERIKALI imesema itaendelea kuchukua hatua kali kwa taasisi zote zininazotoa huduma za fedha kinyume cha sheria kwa kutoa mikopo umiza (kausha damu) na kuwakandamiza wananchi.
Onyo hilo limetolewa leo Disemba, 10 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu wakati akizindua Jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024.
Amesema taasisi hizo zimekuwa zikiwaumiza wananchi kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa pamoja na kupanga njama za kuwafilisi wale ambao wanajua wazi hawatoweza kulipa mikopo hiyo.
“Lazima wananchi wajue kutoafautisha kati ya Taasisi rasmi na hizo zisizo rasmi, lazima tuwaoneshe wananchi kuwa hawako salama wanapokopa kwenye taasisi zisizo rasmi na kuwahamasisha kuwa benki ni salama zaidi”, amebainisha Dk. Nchemba.
Amewataka wadau wa Sekta ya Fedha hususan benki kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kutumia huduma rasmi za fedha kwa kutumia taasisi ambazo zimesajiliwa ili kuepukana na madhara wanayokumbana nayo katika taasisi nyonyaji zinazotoa mikopo umiza (kausha damu).
Amesema ni vema wadau wa Sekta ya Fedha wawaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia benki kupata mikopo pamoja na kutunza fedha zao kwa kuwa kutunza fedha benki ni utaratibu wa kisasa wa uendeshaji wa uchumi.
“Bado kuna baadhi ya maeneo wananchi wanaogopa kuweka fedha benki, kwa kuwa nyinyi mpo kwenye Sekta hii mshirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaeleza wananchi kuwa wasiogope kuweka fedha benki,” amefafanua Dk. Nchemba.
Amesema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kukusanya kodi kwa weledi na kwa kufuata sheria bado wananchi hawajaeleweshwa vizuri kuhusu kuweka fedha benki.
Amewaagiza viongozi wa Taasisi za Fedha nchini kujiridhisha kabla ya kuruhusu watumishi na madalali wao kupiga minada ya mali za wadaiwa mikopo kwenye Taasisi zao kwa kuwa kuna taarifa kuwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu hushirikiana na watu wengine kuwadhulumu mali zilizowekwa kwama dhamana na kuwatia watu umasikini.
”Kuna baadhi ya maeneo hakufanyiki vizuri katika kudai mikopo, mteja amelipa mkopo wake kwa asilimia 80, amebakiza asilimia 20, anatokea mteja mwingine anapenda dhamana ya mkopo iliyowekwa, benki inaamua kupiga mnada wa muda mfupi ambao wanajua mteja hatoweza kulipa ili wamfilisi, mtu amelipa mkopo kwa asilimia 80 halafu unauza dhamana yake ili kufidia asilimia 20 ambayo hajalipia huko ni kumtia umaskini, huu sio utaratibu mzuri wa kujenga sekta ya fedha na sio utaratibu mzuri wa kujenga ustawi wa jamii,” ameongeza Dk. Nchemba.
Dk. Nchemba ameziagiza Benki kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa benki wasio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wateja kuongeza mikopo chechefu.
Aidha, amewaagiza wadua wa Sekta ya Fedha kuendelea kuwasisitiza wananchi kuwa fedha za mkopo zitumike kwenye shughuli za uzalishaji kwa sababu shughuli zinazoweza kuzalisha ndio zinazoweza kurejesha mkopo huku akitolea mfano nchi inapokopa fedha zinapelekwa kwenye miradi mahusi ya maendeleo, kwasababu miradi ya maendeleo ndio inaweza kuzalisha na kulipa deni na haijawahi kukopa kwa ajili ya kulipa mishahara.
Amesema kutokana na kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo ndio maana Tanzania ni miongoni mwa nchi mbili pekee barani Afrika zenye uhimilivu wa deni na kwa Afrika Mashariki na nchi zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania inaongooza.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mwakani Serikali itaanzisha Mtaala Mpya wa masomo ambapo somo la masuala ya fedha na ujasiriamali litakuwa ni la lazima ili kuwaezesha wanafunzi watakapo maliza masomo yao kuweza kujiajiri.
Amewataka wadau mbalimbali kuendelea kutoa maoni kuhusu mtaala huo ili kuuwezesha kufikia lengo kusudiwa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba amesema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha nchini imeandaa Jukwaa la wadau wa Sekta ya Fedha ili kubadilishana mawazo na uzoefu, kupeana taarifa, kujengeana uwezo, kushirikishana katika mafanikio na changamoto na kutafuta suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazoikabili sekta ya fedha nchini.
Amesema malengo ya Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka mitatu (2020/21-2023/24) na kushirikishana mbinu bora za kiutendaji na uzoefu katika Sekta ya Fedha.
Dk. Mwamba amesema malengo mengine ni kujadili fursa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuboresha sekta ya Fedha pamoja na kushirikishana namna bora ya kukuza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi ili kukuza na kuimarisha Sekta ya Fedha.
Ameongeza kuwa Jukwaa hilo pia linalenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa Sekta ya Fedha na kuufahamisha Umma juu ya hatua za maboresho mbalimbali ya kisera na kisheria yaliyofanyika ili kuimarisha Sekta ya Fedha nchini.