Home KITAIFA DK. MWINYI: ZANZIBAR KUWA NA UMEME WA UHAKIKA KUTOKANA NA...

DK. MWINYI: ZANZIBAR KUWA NA UMEME WA UHAKIKA KUTOKANA NA KUTANUKA KWA SHUGHULI ZA UCHUMI

Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inadhamiria kuwa na umeme wa uhakika kutokana na kutanuka kwa shughuli za uchumi, miradi mikubwa ya maendeleo, ongozeko la hoteli za kitalii na kasi ya uwekezaji inayokuwa kila siku.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Disemba, 7 2024 Ikulu – Zanzibar alipozungumza na Ujumbe kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Rita Laraujinha Mkurugenzi Mwendeshaji wa masuala ya nje, Kanda ya Afrika waliomtembelea.

Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa kwa muda mrefu Zanzibar imekua ikipokea megawatt 100 za umeme kutoka Tanzania Bara kupitia waya za chini ya bahari ambao kwa sasa hautoshelezi, hivyo kuna kila sababu ya kupata umeme mbadala na kufikiria kuwa na umeme wa jua, mawimbi au upepo, hivyo ameuomba Umoja wa Ulaya (EU)kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kwenye eneo hilo.

Aidha, amesema, Serikali inafikiria kuzisarifu taka kwaajili ya kupata umeme mbadala hatua aliyoielezea mbali yakupata nishati hiyo lakini pia itadhibiditi taka kwani kumekua na changamoto kubwa ya usimamizi wa taka zinazozalishwa kila siku.

Akizungumzia uwezeshaji wanawake kiuchumi Dk. Mwinyi ameeleza nia ya Serikali kuwaongezea nguvu, uwezo na utaalamu kwa wakulima wa mwani ambao asilimia 90 ni wanawake, kwa kuliinua zao hilo pamoja na kuanzisha viwanda vidogovidogo na vya kati ili kuusarifu na kuzalisha bidhaa zinazotokana na zao hilo kwa kuziongezea thamani badala ya kuuza mwani kama malighafi.

Hivyo, amewashawishi wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya, kuja nchini kuanzisha viwanda vya kuusarifu mwani na kuzalisha bidhaa za zao hilo.

Rais Dk. Mwinyi ameusisitiza Umoja wa Ulaya kuiungamkono Zanzibar katika azma yake ya kukuza Uchumi kupitia sekta za kimkakati ikiwemo Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni Sekta za kipaumbele kwa Serikali anayoiongoza.

Amebainisha kuwa kwa sasa Zanzibar inafanya utalii wa kisasa unaoshajihisha utalii wa kumbi za mikutano, utalii michezo na wa afya ambapo awali ilijikita zaidi kuendesha utalii wa fukwe na maeneo ya urithi ambao umezoeleka kwa muda mrefu.

Akizungumzia masuala ya uwekezaji amezikaribisha nchi za Umoja wa Ulaya, hususan sekta binafsi kuja Zanzibar kubaini fursa za uwekezaji ziliopo kwani kuna maeneo mengi hayajafikiwa hasa kwa sekta ya Uchumi wa Buluu kupitia Utalii, Bandari, Mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini.

Pia, Dk. Mwinyi amegusia masuala ya jinsia na kueleza kuwa Serikali anayoiongoza inafanya kila juhudi kuhakikisha inaweka uwiano sawa kwa wananwake na wanaume kwa nyanja zote za Elimu, Uchumi, siasa na ustawi wa jamii na kuuomba Umoja wa Ulaya kuja kuungamkono kwenye maeneo ya taaluma, kuwajengea uwezo wanawake kwa dhamira ya kuwainua kiuchumi.

Naye, Rita Laraujinha ameipongeza Zanzibar kwa ushirikiano wanaoutoa kwenye Miradi inayosimamiwa na EU na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa wataendelea kuiunga mkono Zanzibar wa kuleta maendeleo hasa kwa masuala ya afya, elimu na Uchumi wa Buluu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here