đź“Ś Dk. Biteko Ahimiza Wadau Kuchangia Ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi
đź“ŚAwashukuru Wadhamini wa UDSM Marathon
Dar es Salaam
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Doto Biteko ameeleza amefurahishwa kwake na uendeshaji wa UDSM Marathon na kusema kuwa inasaidia kufanikisha malengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kutoa elimu bora na kuboresha mazingira ya wanafunzi.
Dk. Biteko amesema hayo leo Desemba 7, 2024 mara baada ya kushiriki mbio hizo za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM MARATHON) zilizofanyika chuoni hapo.
“ Ni dhahiri kwamba mbio hizi zimekuwa muhimu kwa Chuo hiki na jamii kwa ujumla. Tukio hili limeleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Dk. Biteko.
“Natambua kwa misimu mitano mbio hizi zimekua zikichangia katika ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi kinachojengwa hapa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Nyerere Mlimani. Ujenzi wa kituo hiki ulianza kwa michango kutoka kwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na washirika mbalimbali wa maendeleo ya elimu ambapo jumla ya shilingi bilioni 4.4 zimechangwa kutoka kwa wadau,”ameongeza.
Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilishwa kwa kutumia fedha za ndani na hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kukamilisha awamu ya pili ili kutimiza ndoto ya kuwa na Kituo cha Wanafunzi kitakachowezesha wanachuo kuwa na maeneo ya kujifunzia na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Ujenzi wa awamu ya pili unahitaji shilingi bilioni 3.3 na hivyo kufanya gharama za ujenzi kwa awamu hiyo kufikia shilingi bilioni 9.4 badala ya shilingi bilioni 6 zilizokadiriwa awali ambazo zimebadilika kwa sababu mbalimbali.
Akiwahakikishia ushiriki wake katika kufanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo Dk. Biteko amesema “Nataka niwatoe wasiwasi kuwa jambo hili ni letu sote kwa kuwa majengo haya yatatumika kwetu sote. Nalibeba suala hili kwa uzito wake ili kilichoahidiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kipatikane kwa wakati,”
Pia, ametoa wito kwa wadau mbalimbali
kuunga mkono jitihada za kuwezesha mbio hizo kufanyika kwa ustadi mkubwa na kwa kuwa zimeonesha kupitia mshikamano, wanaweza kufanikisha malengo makubwa ya kijamii na kielimu. Sambamba na kuhimiza uongozi wa Chuo kuandaa namna ya kukutanisha wadau zaidi ili kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo.
Vilevile, Dk. Biteko amempongeza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa usimamizi wake katika shughuli za maendeleo ya Chuo hicho.
Kwa upenda wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Chuo hicho kinathamini mchango wa Serikali katika ujenzi wa Kituo hicho cha wanafunzi.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (Utawala na Fedha), Profesa Bernadeta Kilian amesema Chuo hicho kilianzisha ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya kupumzika na kukuza uwezo wa kubuni au kupata mawazo Mapya.