📌 Asema CCM Inaweza Kazi, Ipewe Kura
📌 Wabunge Waeleza Mafanikio ya CCM Mara
📌 Wagombea Uenyeviti Wajinadi kwa Wananchi
📌 Wananyamongo Waahidi Ushindi CCM Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Mara
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Dk. Biteko ameyasema hayo leo Novemba 20, 2024 wakati akifungua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mara zilizofanyika katika Mji wa Nyamongo Wilaya ya Tarime.
Ameeleza kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi wala kuvunjiana heshima na kuwa wananchi hao washinde ubaya kwa wema.
Aidha, Dk. Biteko amefika eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wa Nyamongo wachague watu ambao wataungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo.
“Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida za watu na kuzitatua,” amesema Dk. Biteko.
Amebainisha kuwa uchaguzi huo ni muhimu na sio wa majaribio hivyo ni lazima wananchi wachague viongozi ambao sio walalamikaji na kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi bali kwa kufanyakazi.
“CCM tumekuja hapa kuwaomba kura zenu si tu kwa sababu huu ni msimu wa kuomba kura umefika ila kazi tunaweza kuifanya, tumeshaifanya na tuna cha kuonesha, mtakumbuka mwaka 2020 tulikuja na ilani na kusema tutakayoyafanya na tumeeleza hapa tuliyoyafanya,” amesisitiza Dk. Biteko.
Amesema kuwa licha ya kufanya siasa ni lazima viongozi wajue wajibu wao ni kuwaletea wananchi maendeleo akitolea mfano namna kijiji cha Nyamongo kilivyolipwa shilingi bilioni nne ikiwa ni fidia kwa wananchi.
Amefafanua kuwa Rais Dk.Samia ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kuwa na maisha nafuu hivyo wananchi wa Nyamongo wamuunge mkono kwa kuchagua wagombea wa CCM.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kuna fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa jamii (CSR) zinazohitaji kibali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha kibali hicho kinatoka kabla ya mwisho wa juma hili ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika kwa kupata miradi ya maendeleo.