Home KITAIFA WATENDAJI WAZEMBE TANESCO KUANZA KUCHUKULIWA HATUA KILA MWEZI – DK. BITEKO

WATENDAJI WAZEMBE TANESCO KUANZA KUCHUKULIWA HATUA KILA MWEZI – DK. BITEKO

📌Asisitiza Kituo cha Huduma kwa Wateja kuongeza ufanisi

📌Tathmini kufanyika kwa Mkataba wa Mtoa Huduma kwa wateja TANESCO

📌 Mameneja wa Mkoa TANESCO kupimwa kwa matokeo

📌TANESCO yatakiwa kujenga taswira nzuri ya nchi

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko ameagiza ripoti ya taarifa kila wiki ya Kituo cha Huduma kwa Wateja ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ianze kutolewa kila mwezi ili kufahamu maeneo yenye changamoto ya umeme nchini na kurahisisha watendaji wazembe kuchukuliwa hatua kwenye maeneo hayo.

Dk. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye kituo hicho cha huduma kwa wateja leo Aprili, 4 2024 jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi wa kituo hicho muhimu kwa wananchi nchini.

“Wateja wote wanaopiga simu kwa sababu mnaletewa matatizo ya wananchi ni lazima mtengeneze kila wiki tupate ripoti ni mkoa gani wanahudumiwa wateja kwa haraka na mkoa upi haupewi huduma kwa haraka ili tuchukue hatua,” amesisitiza Dk. Biteko.

Ameagiza kila mkoa nchini uliopo chini ya TANESCO ufanyiwe tathmini kujua umeme umekatika mara ngapi na kufahamu sababu zilizopelekea umeme kukatika katika maeneo hayo ili kama ni uzembe umefanyika Serikali iweze kuchukua hatua haraka.

“Mimi ninafahamu kuna wakati umeme unakatika sio kwa sababu ya matatizo makubwa bali ni kwa matatizo madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini zetu.

Unakuta kuna mahali mti umedondoka kwenye njia zetu na unachukua muda mrefu kuondolewa, au mteja amepiga simu anachukua muda kuhudumiwa, tunahitaji hiyo ripoti,” amesisitiza Dk. Biteko.

Katika hatua nyingine Dk. Biteko ameagiza, kituo kuangalia utaratibu wa namna nzuri ya wateja kutogharamia malipo kipindi wanapopiga simu kuhudumiwa na kituo.

“Kiu yangu ni kuona kwamba tunakuwa na mfumo wa kupiga simu kwa Wateja bila ya kuwaingiza kwenye gharama kwa sababu kuwaingiza kwenye gharama haina maana yoyote kwa wanachi,” ameongeza Dk. Biteko.

Dk. Biteko amemuagiza Meneja wa Kituo hicho kuhakikisha taarifa ya Maendeleo ya kituo hicho kwa kila mkoa inawasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati ili kuongeza ufanisi wa watendaji nchini na asipofanya hivyo atafanyiwa mabadiliko katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

Vile vile, ameagiza TANESCO kuhakikisha inajenga taswira nzuri ya nchi kupitia watendaji wa Shirika hilo kupitia kituo hicho.

Amesema fedha zilizotolewa na Serikali za dharura kiasi cha shilingi bilioni 2.9 watu wahudumiwe ili kufurahia kuwa Watanzania kwa kupata huduma bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here