Pwani
WAKULIMA wadogo wa zao la mpunga nchini wametakiwa kutumia wataalamu wa kilimo walio katika ngazi ya vijijini na kata ambao ni Maafisa kilimo na Maafisa Ugani, ili waweze kufanya maboresho kuanzia hatua ya awali ya zao la mpunga ili zao hilo listawi vizuri na kuwaletea manufaa hapo baadae.
Wito huo umetolewa Novemba,6 2024 na Mkuu wa divisheni ya kilimo na Uvuvi wilaya ya Bagamoyo, Gerald Mwamuhamila, wakati akifunga matunzo ya uzalishaji wa mbegu zenye ubora za mpunga mafunzo hayo yalioandaliwa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI) kuvikutanisha vikundi 13 vya uzalishaji mbegu kutoka mikoa mbalimbali, nchini.
“Walichojifunza hapa ni kwaniaba ya wakulima nchi nzima kuendelea kuwasaidia wenzao kupata elimu katika uzalishaji. Tunaendelea kusisitiza kuendelea kubadilisha uzoefu na wataalamu waliopo maeneo yao na ndio madaktari wa mazao,”amesema.
Naye Afisa Utafiti wa Mifumo ya Mbegu nchini Kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mbegu ya mpunga (IRRI), Martine Ndomondo, amesema mafunzo yaliyotolewa yalikuwa yanawahusu wanawake na si wanaume ili kuwawezesha wanawake kiuchumi ni wakulima wadogo kulima kilimo cha kisasa na wajikwamue kiuchumi.
Kwa upande wake Beatrice Swai kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) amesema kuwa wakulima waliopata bahati ya kupata mafunzo, waende kueneza ujuzi waliupata ili kuwanufaisha wakulima wengi zaidi nchini.
Amesema wamejifunza sheria mbalimbali za mbegu na kutunza mbegu TOSCI itakuwa pamoja nao wakati wanawahitaji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka mikoa ya Mbeya na Rukwa wamesema kuwa, wanawashukuru wakufunzi kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwani wataacha kufanya kilimo cha mazoea.
Jumla ya washiriki 35 wameshiri mafunzo hayo kutoka katika vikundi 13 vya uzalishaji wa mbegu katika Wilaya ya Bagamoyo na wawakilishi wa vikundi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es salaam, Mbeya, Morogoro, Rukwa na Katavi.