Pwani
WADAU wa kilimo wametakiwa kujitokeza kutoa elimu ya uzalishaji mbegu kwa wakulima wa mpunga ili kuondokana na changamoto ya uzalishaji mbegu nchini pamoja na kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Akizungumza Novemba, 4 2024 wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu ya uzalishaji wa mbegu za ubora wakuazimia (UKU) za mpunga iliyofanyika wilayani Bagamoyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga( IRRI) na kuvikutanisha vikundi vya uzalishaji mbegu kutoka mikoa mbalimbali ,Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Wilaya ya Bagamoyo Gerald Mwamuhamila amesema ni wakati wa wadau sasa kujitokeza na kuokoa sekta hiyo kwakufundisha wakulima kutengeneza mbegu ambazo zitazalisha mpunga bora.
“Lengo la mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuzalisha Mbegu za kuazimia ubora na kufanya hivyo ni kutatua changamoto ya upungufu wa mbegu za mpunga ambayo ipo inawakabili wakulima mbalimbali.
“Kupitia mafunzo haya maanaake wakulima hawa watakuwa wamerudi kwenye maeneo yao watakuwa na jukumu la kuzalisha mbegu zilizo bora,ili kufanikisha hilo tunatoa kwa wadau wanaofanya kazi kama IRRI watusaidie kupanua wigo za taasisi za uzalishaji kwa kutoa elimu kwa wakulima mbalimbali wa mazao mengine ili wapate wawezeshaji ili kuondokana na changamoto ya mbegu nchini,”amesema Mwamuhamila.
Amesema wazalishaji wa mazao yakiwemo mpunga ni wengi nchini lakini suala la mbegu zenye ubora limekuwa changamoto na badala yake watu wengi wamekuwa wakizalisha mpunga kwa mbegu zinajirudia na kusababisha uzalishaji unakuwa chini tofauti na mwanzo.
“Mfano kwenye kikundi cha kuzalisha mbegu Bagamoyo kwa sasa wanazalisha tani mbili na nusu kwa hekta moja wakati mahitaji halisi kwa mkulima ambaye amezalisha na kuzingatia utaratibu ikiwemo mbegu bora uzalishaji unapaswa kuwa ni kuanzia tani nne ndiyo malengo,kupitia mafunzo haya ifikapo mwaka 2025 na mwakani 2030 wanatarajia mkulima kufikisha tani sita kwa hekta moja,”amesema Mwamuhamila.
Amesema jumla ya washiriki 35 walioshiriki mafunzo hayo kutoka katika vikundi 13 vya uzalishaji wa mbegu kutoka Wilaya ya Bagamoyo wa wawakilishi wa vikundi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es salaam, Katavi,Mbeya na mingineyo.
Amesema baada ya mafunzo hayo wanatarajia wakulima hao watakaozalisha mbegu zinakuwa na idhini ya Wakala wa Mbegu nchini (ASA) pia wanaoruhusu matumizi bora ya mbegu na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu nchini (TOSIC).
Ameongeza kuwa kukupitia semina hiyo mbegu zitakazozalishwa zitawafaa wakulima walioshiriki mafunzo na wengine ambao hawapo hapo na bei yake itakuwa nafuu tofauti kampuni zingine zinazozalisha mbegu hiyo.
Amesema uzaishaji wambegu pia utasaidia kutatua ukosefu wa chakula na wakulima wataongeza uzalishaji ili waweze kuzalisha ziada kupata mapato mengine nje ya chakula.
Naye Afisa Miradi wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo Afrika Mashariki, Robert Mwalubeke amesema lengo la mafunzo hayo ni kuandaa wazalishaji mbegu hasa zenye ubora kwakuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa mbegu na kuwafikia wakulima kwenye mabonde waliopo.
“Mbegu bora kuwafikia wakulima ilikuwa changamoto hivyo tunaongeza elimu ya uzalishaji ili mbegu ipatikane kwa wakati sahihi,hapa tunaandaa wazalishaji katika maeneo mbalimbali ili wazalishe mbegu zenye ubora kuwauzia wakulima waliopo maeneo husika,”amesema
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini na upatikanaji wa mbegu bado hauridhishi.
“Zaidi ya wakulima asilimia 70 wanarudia mbegu na chini ya asilimia 30 wanapanda mbegu mpya hiyo ni fursa,hasara za kurudia mbegu ni pamoja na mavuno kuwa madogo kupata mbegu haina ubora na mpunga ukivuna hauna ubora na kupunguza kipato kwa mkulima,”amesema.
Kwa upande wake mshiriki kikundu cha Tuinuane Kiuchumi kutoka Rukwa, Neema Japhet amesema wao wanajishughuli na kilimo cha mpunga na kupitia mafunzo hayo wanaamini watafanya kilimo chenye tija zaidi.
Amesema lengo la kushiriki mafunzo hayo ni kujifunza jinsi ya kuandaa mbegu bora za mpunga hivyo wanatarajia kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa mkoa huo ili waweze kuzalisha kwa wingi mbegu.