Home KITAIFA JENERALI MUSUGURI AMEACHA ALAMA YA UZALENDO NA KUJITOA KWA AJILI YA TAIFA...

JENERALI MUSUGURI AMEACHA ALAMA YA UZALENDO NA KUJITOA KWA AJILI YA TAIFA : DK. BITEKO

đź“Ś Serikali itaenzi na kuthamini mchango wake

đź“Ś Asema Jenerali Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki na amani na usalama

đź“Ś Asema alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa

đź“Ś Aiasa jamii kuacha alama katika maisha ya kila siku

đź“Ś Dkt. Biteko aongoza mamia ya watu mazishi ya Jenerali Musuguri Butiama

Mara

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano pamoja na kuifundisha jamii moyo wa dhati wa kuilinda nchi.

Dk. Biteko amesema hayo leo Novemba 4, 2024 Butiama mkoani Mara wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Jenerali Mstaafu Musuguri.

“ Katika uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo, baba huyu ameacha alama ya uzalendo, kujitoa kwake na kuipenda nchi pia aligeuza changamoto kuwa fursa. Musugurli alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa lake, tujiulilize sisi tuliobaki tutaacha alama gani? yeye aliacha ya kulikomboa Taifa letu,” amesema Dk. Biteko.

“ Alikuwa kiongozi aliyetamani amani na alisisitiza hakuna vita iliyo nzuri aliamini nguvu ya mshikamano na katika kipindi hiki tunachoelekea cha uchaguzi tushikamane, tushirikiane na kuendelea kufanya amani iwe tunu ya Taifa letu,” amesisitiza Dk. Biteko.

Amesema Serikali itauenzi mchango wake daima na kutaja baadhi ya heshima alizowahi kupewa ikiwa ni pamoja na kutunukiwa medali mbalimbali mfano ya Vita ya Kagera na kuwa Serikali itaendelea kusimamia ujasiri, uzalendo na kuthamini amani.

Vilevile, ameihimiza famili ya Jenerali Mstaafu Musuguru kurithisha vizazi vyao mema yake pamoja na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao sambamba na kuwashukuru madaktari wote waliomtibu wakati akiugua.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax wakati akimkaribisha Dk. Biteko kuzungumza amesema kuwa Taifa limepoteza hazina na kamwe Jenerali Musuguri hatasahaulika kwa mema yake yote na kuwa Jeshi litaenzi mchango wake.

Naye, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda amesema kuwa kifo cha Jenerali Musuguru ni msiba mkubwa si tu kwa Jeshi bali kwa Tanzania yote kulingana na mchango wake wa ulinzi alioutoa katika utumishi wa umma kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

“Alishiriki Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilimjenga, kumkomaza na kumpa uzoefu mkubwa ambao aliporejea nchini alitumia kwa ajili ya kujenga nchi yake na kuandaa mipango mbalimbali ya kivita ambayo nchi yetu ilishiriki ikiwa ni pamoja na vita vya mvamizi Iddi Amini na vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.” Ameeleza Jenerali Mkunda.

Akihubiri wakati wa misa hiyo ya mazishi, Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Musoma, Michael Msonganzila amesema kuwa makundi mbalimbali ya watu yamekusanyika eneo hilo kwa ajili ya kumuaga Jenerali Mstaafu Musuguri na kuwa wameunganishwa na Jenerali huyo katika tukio hilo.

“Kilichotukutanisha ni misa ya kumuombea Musuguri aende kwa safari ya amani kuelekea huko kwa aliyetuumba na alituumba tumjue, tumpende na tumtumikie na mwishowe twende kwake mbinguni” amesema Askofu Msonganzila

Ameendelea kusema “ Kumuombea Jenerali huyu ni tendo la kiimani, tunaamini Yesu alikufa, akazikwa na kufufuka na pia tunaamini Mungu atawakutanisha wote waliokwisha fariki na Yesu Kristo”

Askofu Msonganzila amebainisha kuwa mkusanyiko mkubwa wa watu unafanya watu watafakari kwa kina juu ya uhai wake na kuwa Jenerali Musuguri alikuwa mnyenyekevu, shupavu na kuwa alipigana vita vya haki wakati ambao Nduli Iddi Amin kutoka Uganda alivamia Tanzania mwaka 1978.

Kiongozi Mkuu wa Kabila la Zanaki, Chifu Japheti Wanzagi amesema kuwa Jenerali Musuguri alikuwa na sifa kadhaa ikiwemo unyenyekevu na mtu wa aina ya pekee ambaye alimjali na kumthamini na kusaidia kila mtu.

“Mzee huyu hakuwa na ukwasi wa mali bali utajiri wa utu wema, wengi wetu tulipenda kukaa nae na kuzungumza nae mara kwa mara. Kwa ujumla tunamshukuru Mzee kwa ukarimu na moyo wake wa kusaidia wahitaji,” amesema Chifu Wanzagi.

Jenerali mstaafu David Bugozi Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 kijijini kwake Butiama na kufariki Oktoba 29, 2024 katika hospitali ya rufaa Bugando iliyopo Mwanza.

Alitumikia Jeshi kwa miaka 43 ambapo alihitimu kozi mbalimbali za Jeshi na kuwa Jenerali mwaka 1985. Aidha, mazishi yake yaliambatana na upigwaji wa mizinga ya heshima 17.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here