Home KITAIFA TMA YATOA TAHADHARI MWELEKEO WA MVUA MSIMU WA NOVEMBA 2024 HADI APRILI...

TMA YATOA TAHADHARI MWELEKEO WA MVUA MSIMU WA NOVEMBA 2024 HADI APRILI 2025

Dar es salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Nchini ( TMA) imewashauri Wakulima kutumia taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi kulingana na utabiri wa msimu.

Pia wakulima na maafisa ugani wameshauriwa kuendelea kutumia utabiri wa siku na siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu unaotolewa na Mamlaka hiyo.

Ushauri huo umetolewa leo Jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk. Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za Msimu wa Novemba, 2024 hadi Aprili 2025.

Dkt Chang’ amesema kuwa Mvua hizo zimeanza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini kama ilivyotabiriwa nakwamba maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki yameendelea kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu.

Aidha,meendelea kufafanua kuwa utabiri wa mvua za Vuli unatarajiwa kuendelea kama ulivyotabiriwa ambapo Mwelekeo wa mvua za Msimu wa Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025, Mvua hizo ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.

“Maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba na kuisha kati ya mwezi Aprili na Mei ya mwaka unaofuata,Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa kama ilivyoelezwa katika kipengele cha 2 cha taarifa hii, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa” amesema

Nakuongeza kuwa “Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

Aidha amesema mvua nyingi zinatarajiwa katika kipindi cha nusu ya pili ya msimu kuanzia Februari – Aprili, 2025 ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya Mwezi Novemba, 2024 hadi Januari 2025.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi mkuu huyo wa TMA amesema kuwa Mifugo na Uvuvi katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki.

Hata hivyo amesema milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo, na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza.

Pia amesema upungufu wa mvua hasa katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2024 hadi Januari, 2025) unatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

“Wafugaji wanashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo,wafugaji na wavuvi wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa na maofisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kutokea na kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa.”amesema Dr.Chang’a

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here