Asisitiza hakuna sababu ya kumficha mtoto mwenye ulemavu
Kilimanjaro
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni 20.21 kwa ajili ya watu wenye ulemavu ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu na isiyokuwa na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Amesema hayo leo Ijumaa, Oktoba 25, 2024 alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe na Miaka 60 ya Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), Mkoani Kilimanjaro.
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Halmashauri zilitenga shilingi bilioni 16.14, hili ni ongezeko kubwa. Viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu wekeni utaratibu ili wanachama wenu waweze kunufaika na fursa hii ambayo Serikali imeitoa kwa watu wenye ulemavu,”amesema.
Aidha,Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi (UNOPS)imewezesha kupatikana ruzuku ya shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuwapima watoto wasioona na viziwi.