Dar es Salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) leo Oktoba,21 2024 imeanza rasmi kambi maalum ya upasuaji rekebishi ambayo itahitimishwa Novemba, 1 mwaka huu kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma za upasuaji rekebishi (Rafiki Surgical Mission) kutoka nchini Australia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema kambi hii inahusisha wagonjwa wote wenye ulemavu wa mikono na miguu au sehemu yoyote ya mwili ambayo inatokana na ajali mbalimbali ikiwemo ajali za moto, ajali za barabarani au ulemavu wa kuzaliwa nao pia sehemu zilizotolewa uvimbe au saratani za ngozi zinazohitajika kufanyiwa upasuaji rekebishi.
“Lengo la kambi hii ni kubadilishana uzoefu na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzetu lakini pia kupitia kambi hii ni fursa sisi kama hospitali ya taifa kushirikisha ujuzi huo kwa madaktari wengine nchini ili tuweze kuwasaidia wananchi wenye changamoto mbalimbali ili kuepuka kutumia gharama kubwa kwenda nchi za nje kufuata matibabu,” amesema Profesa Janabi.
Kwa upande wake Daktari wa Upasuaji Rekebishi MNH, Dk. Edwin Mrema amesema wagonjwa 33 watafanyiwa uchunguzi wa awali ili waweze kuandaliwa kwa ajili ya upasuaji rekebishi kutokana na changamoto walizonazo.