Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
BALOZI wa Hungary hapa nchini mwenye Makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya, MZsolt Mészáros, ameipongeza Tanzania kwa kusimamia vema sera zake za fedha na uchumi, hatua iliyoifanya iendelee kuimarika kiuchumi na kuahidi kuwa nchi yake itaongeza ushirikiano kwa faida ya nchi hizo mbili.
Mészáros ameyasema hayo, Oktoba, 5 2024 alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba Katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Amasema kuwa nchi yake imekuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania ikiwemo hatua kubwa inazochukua kuvutia uwekezaji wakiwemo wanaotoka nchini mwake.
Aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuchangia maendeleo yake hususan katika sekta za huduma za jamii kama vile maji kupitia mpango wake maalumu wa kushirikiana na Serikali ujulikanao kama Tied Aid Facility.
Akizungumza na Balozi huyo wa Hungary, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa uchumi wa Tanzania umeimarika ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, uchumi umekua kwa wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5 katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Amesema kuwa makadirio ya ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2024/2025 ni wastani wa asilimia 5.4 na asilimia 5.8 mtawalia, kufuatia miongozo na usimamizi mzuri wa uchumi, wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwezi Agosti mwaka 2024, zinaonesha kuwa uchumi wetu umeimarika licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali huku ukuaji huo ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta za ujenzi, kilimo, fedha na sekta ya bima,” amesema Dk. Nchemba.
Aidha, Dk. Nchemba amemweleza Balozi huyo kuwa kasi ya mfumuko wa bei imedhibitiwa na kuwa katika kiwango wa tarakimu moja cha asilimia 3.1, kiwango ambacho kimekubaliwa pia katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizoweka ukomo wa asilimia 8 na kiwango cha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) cha asilimia 3 hadi 7.
Amesema kuwa uimara wa uchumi wa Tanzania umethibitishwa pia na mashirika yanayofanya tathimni ya uwezo wa nchi kukopesheka duniani, ikiwemo Taasisi ya Moody’s ambayo hivi karibuni, iliipandisha Daraja Tanzania kutoka Daraja B2 kwenda Daraja B1 pamoja na Taasisi ya Fitch ambayo imeipa Tanzania Daraja B+ yenye Mtazamo Chanya (positive Outlook).
Dk. Nchemba amesema kuwa hatua hiyo imeifanya Tanzania na sekta binafsi kuaminiwa zaidi na taasisi za fedha za kimataifa kwamba zinaweza kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa na kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Hungary kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali watakayo ona yanawafaa kutokana na Serikali kuweka mazingira bora yanayovutia uwekezaji.