Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema kukamilika kwa miradi mikubwa mitatu ya Ujenzi wa jengo jipya ya wagonjwa wa nje (OPD), Ukarabati wa lililokuwa jengo la hospitali ya Tumaini na ujenzi wa kituo cha utengamao Mbweni kutawezesha wagonjwa 1,500 wa nje kuhudumiwa kwa siku.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk. Lemeri Mchome amebainisha hayo leo Oktoba 3, 2024 katika kikao cha tano cha baraza la tano la wafanyakazi wa MOI kinachoendelea ukumbi wa APC uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.
“Katika jitihada za kupunguza msongamano na kuboresha huduma kwa wananchi, kwa kupitia Wizara ya Afya, MOI inatekeleza miradi mikubwa mitatu ikiwemo ya ujenzi wa jengo jipya la OPD, ukarabati wa lililokuwa Hospitali ya Tumaini na ujenzi wa kituo cha utengamao cha Mbweni…miradi hii yote ikikamilika itawezesha wagonjwa zaidi ya 1,500-3000 kuhudumiwa kwa siku” amesema Dk. Lemeri
Amesema pia miradi hiyo itaongeza idadi ya wagonjwa watakaolazwa kutoka 362 hadi kufikia zaidi ya 500 na hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MOI Profesa Charles Mkony amewataka watumishi wa MOI kuendea kuwa wabunifu katika kutoa matibabu ili wagonjwa waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kawaida.
“Ni lazima jamii ifahamu kuwa MOI inatoa matibabu ya kipekee kabisa tofauati na maeneo mengine, huduma zake ni za kipekee na zinahitaji ubunifu zaidi ili kuwawezesha wagonjwa kupona haraka” amesema Profesa Mkony na kuongeza
“Wakati menejimenti wakiendelea na uboreshaji wa maslahi ya watumishi na miundombinu ya kufanyia kazi, niwaombe watumishi endeleeni kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa, sijasikia kwa siku za hivi karibuni na ndiyo maana nasema endeleeni hivyo”