Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amekutana na waendesha pikipiki za abiria ” bodaboda” na kuwakumbusha ahadi yake ya mkopo nafuu wa pikipiki.
Akizungumza na uongozi wa wasafirishaji hao pamoja na baadhi ya waendeshaji leo oktoba 2 amesema fursa bado ipo na ametoa siku 30 kupata pikipiki kwa wale watakaokamilisha taratibu.
Amesema alipokuwa akikabidhi vyeti baada ya mafunzo ya udereva chuo cha Veta Musoma aliahidi kudhamini mkopo wa pikipiki kwa kianzio cha shilingi laki tatu kutoka benki ya Azania lakini muitikio umekuwa mdogo.
Mathayo amesema dhamana aliyoiomba Azania ni ya pikipiki 200 lakini ni zaidi ya miezi 2 ni watu 2 tu ambao wametimiza masharti.
Amesema kwenye masomo ya udereva aliyoyafadhili yalikuwa na muitikio mkubwa lakini kwenye kupata pikipiki kwa mkopo nafuu kumekuwa na kusuasua.
” Ndugu zangu tunajikwamisha wenyewe kupata fursa zilizopo kutokana na kuto kuzingatia utaratibu.
” Tulikubaliana kuwa kwenye vikundi vya watu watano na kuwa na kianzio cha laki 3 nami nidhamini kule benki ili kupata pikipiki lakini mmeshindwa sasa natoa nafasi nyingine,”amesema.
Amesema nafasi ya mwisho anaitoa kwa wanaohitaji hata wasipofika 200 kwa muda walioutoa wafike ofisi ya bodaboda Wilaya ili kuanza utaratibu kwa muda uliotolewa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waedesha Pikipiki Wilaya ya Musoma, Stephano Silasi amesema wamepokea maagizo ya mbunge Mathayo na wanaendelea kuhamasisha madereva ufatilia mkopo wa pikipiki.
Amesema mbunge Mathayo amekuwa akifanya jitihada za kusaidia makundi ya wananchi na yeye kama Mwenyekiti wa waendesha pikipiki atamsaidia kwenye eneo hilo.