Dar es Salaam
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) imesema tayari wapangaji 648 wamepewa notisi za kulipa kodi,huku zoezi la kuwaondoa linatarajiwa kuanza Oktoba 7, 2024, likiratibiwa na dalali wa Mahakama, Twins Action Mart.
Pia TBA imejipanga kuchukua hatua kali dhidi ya wapangaji wanaoshindwa kulipa kodi ya pango kwa wakati, kwani hali hiyo inakwamisha mipango ya maendeleo na ukarabati wa nyumba.
Akizingumza leo Oktoba, 2 jijini Dar es Salaam na Waandishi wa Habari Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch Daud Kondoro, amesema kuna malimbikizo ya madeni yanayokaribia shilingi bilioni 14.8.
Amesisitiza kuwa hatua za kisheria zitaxhukuliwa dhidi ya wapangaji hao wakaidi, ikiwa ni pamoja na kuwafungulia kesi za madai. TBA pia inatekeleza mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) ili kuboresha ukusanyaji wa kodi.
Aidha, mpangaji anayeishi kwenye nyumba za TBA atakuwa na fursa ya kulipwa kodi moja kwa moja kutoka kwenye mshahara wake, huku vitasa janja na smart meters vikiendelea kufungwa kwenye majengo yote mapya.
Arch Kondoro alihimiza wapangaji kulipa madeni yao kwa wakati ili kusaidia juhudi za ujenzi wa makazi bora, na aliwataka wananchi kufuatilia taarifa za TBA kupitia mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya wakala.