Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Wizara zenye dhamana ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufanyakazi kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi changamoto za kimazingira na mabadiliko ya tabianchi zinazoibuka maeneo mbalimbali ya nchi.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba, 25 2024 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijaji alieambatana na timu ya watendaji wakuu wa Wizara hiyo, waliofika kujitambulisha.
Amesema, ni vema Wizara hizo mbili kuweka mkazo kuzipitia Sera, kanuni, miongozo, mipango na mikakati ya kudhibiti changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu na kuibua utatuzi wa masuala hayo.
Amesema, uvamizi wa majichumvi kwenye maeneo ya kilimo, visima na makaazi ya wananchi, mporomoko wa fukwe za bahari na ukosefu wa mvua na mvua zisizotarajiwa bado ni matatizo yanayoathiri kwa kiasi kikubwa.
Rais Dk. Mwinyi amewataka watendaji wa wizara hizo kutumia makongamano na mikutano ya kimataifa ya kimazingira kuziwasilisha changamoto hizo zinazoikabili nchi ili kupata ufadhili na rasilimali za kukabiliana nazo.
Aidha, aliwasisistiza kuwa na mipango shirikishi kuanzia ngazi za chini kwa jamii ili nayo itoe mchango wake.
Pia, Dk. Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kuzuia athari za mazingira zisiendelee kuathiri maisha ya watu.
Akizungumzia masuala ya Muungano, Rais Dk. Mwinyi ameridhia ombi la Waziri Kijaji la kutaka siku tatu kila mwezi kwa watendaji wa Wizara hizo mbili kukutana Zanzibar na kuwa na mikutano na wananchi kutoa maoni yao juu ya changamoto za Muungano.
Kuhusu biashara ya kaboni, (gesi ukaa) Dk. Mwinyi aliwataka watendaji hao kushirikiana kwa pamoja, kujengeana uwezo na kuwatafuta wataalamu kwani biashara hiyo ni mpya ulimwenguni.
Pia, amesisitiza suala la Uratibu wa shughuli za Muungano kwani sekta zote wanazozisimamia zinahitaji ushirikiano wa karibu ili kuleta ufanisi.
Naye, Waziri Dk. Kijaji ameeleza kuwa tayari Wizara hiyo imeandaa timu ya wataalamu na imeanza utafiti na kuandika miradi kwa lengo la kuiwasilisha kwa wafadhili ili kupata fedha zitakazoendesha miradi ya kimazingira.
Amebainisha, kuwa uharibifu wa mazingira ni mkubwa hasa katika fukwe unaosababishwa na mmongonyoko na uvamizi wa maji chumvi kwenye maeneo ya kilimo, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kukabiliana na hali hiyo.
Waziri Dk. Kijaji aliteuliwa nafasi aliyonayo sasa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Julai 03 mwaka huu.