Home KITAIFA TANESCO YAANZA RASMI ZOEZI LA KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA MIRADI...

TANESCO YAANZA RASMI ZOEZI LA KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA MIRADI YA UMEME

📌Ni mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 Tunduru -Masasi .

📌Jumla ya shilingi Bilioni 4.7 kutumika kulipa fidia kwa wananchi

📌Wananchi waahidi kuyahama maeneo ndani ya siku 30 walizopewa.

Mtwara

JUMLA ya wananchi 1,526 wanatarajia kunufaika na malipo ya fidia ya shilingi bilioni 4.7 baada ya kupisha mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa Kituo kipya cha kupoza umeme cha Masasi kilichopo Mkoani Mtwara.

Akizungumza baada ya wananchi kukabidhiwa hundi April 26, 2025 Mwenyekiti wa Kijiji cha Sululu Venant Kamtahule licha ya kulishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya malipo hayo, wamesema ujenzi wa miradi hiyo imelenga kuimarisha upatikanaji wa umeme utakaochochea shughuli za kiuchumi na uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho.

‘’Kiukweli tunaishukuru sana TANESCO wananchi wangu takribani 16 wa Kijiji cha Sululu wamenufaika na malipo ya fidia, haya ni mafanikio makubwa tuliyokua tukiyasubiria kwa muda mrefu .Tunaimani mradi huu utaongeza chachu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi,’’ alifafanua ndugu Venant

Naye Meneja wa TANESCO Wilayani Masasi Mhandisi Kidala Maeda amesema zoezi hilo la ulipwaji fidia limeanza tangu April 25, 2025 ambapo amefafanua kuwa hatua hii itamuwezesha Mkandarasi kuendelea na ujenzi hususani katika Kituo cha kupoza umeme cha Masasi ambao utekelezaji wake uko katika hatua za awali.

‘’Kama mnavyojua hii Mikoa miwili ya Lindi na Mtwara bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa tunatumia mashine za gesi kutoka Mtwara, lakini Serikali ikaona ni wakati sasa na sisi watu wa Kusini tupate umeme kupitia Gridi ya Taifa ili tunufaike na umeme unaozalishwa kutoka Mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere ambao umekamilika rasmi’’ amesisitiza Mhandisi Kidala.

Mradi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Masasi utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 70 ambapo jumla ya vijiji 43 vinapitiwa na Mradi huo katika Wilaya za Masasi, Nanyumbu na Tunduru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here