Home KITAIFA RAIS DK.MWINYI : ZANZIBAR ITAHAKIKISHA MUUNGANO UNAENDELEA KUIMARIKA

RAIS DK.MWINYI : ZANZIBAR ITAHAKIKISHA MUUNGANO UNAENDELEA KUIMARIKA

Dodoma

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha Muungano unaimarika kufikia dhamira ya Waasisi wake ya kudumisha Uhuru,Umoja na Mshikamano wa Watanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi ametoa tamko hilo Aprili, 26 2025 alipozungumza katika Hafla ya Kutunuku Nishani za Kumbukumbu ya Muungano ilioambatana na Uzinduzi wa Kitabu cha MWALIMU JULIUS NYERERE PHOTOGRAPHIC JOURNEY cha Historia ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Ameeleza kuwa watanzania wana kila sababu ya kudumisha Muungano kwani ni tunu ya Taifa ya kujifaharisha nayo na ni kielelezo cha Muungano wa Mafanikio Barani Afrika.

Dk.Mwinyi amesema Waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume walikuwa na dhamira thabiti ya kuwaunganisha watanzania kisiasa,kiuchumi na kijamii kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo jambo linalopaswa kudumishwa na kila mtanzania.

Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazozitekeleza za kumaliza changamoto za Muungano kupitia vikao vya majadiliano hadi kubakia changamoto yatu hivi sasa miongoni mwa 25 zilizokuwepo awali.

Akizungumzia uzinduzi wa Kitabu hicho amesema ni kutambua dhamira na mchango wa Mwalimu Nyerere wa kuasisiwa kwa Muungano ambao ni msingi mkuu wa umoja, amani na maendeleo ya watanzania.

Aidha amesema Kitabu hicho kitawasaidia Watanzania waliozaliwa Baada ya Muungano Kujifunza na kumtambua Muasisi Huyo wa Muungano na faida ya Muungano huo tangu Kuasisiwa kwake Miaka 61iliyopita.

Rais Dk.Mwinyi ameipongeza kazi nzuri iliofanywa na watunzi wa kitabu hicho ilioonesha kuthamini mchango wa Baba wa Taifa na kutoa rai ya kuchapishwa kwa wingi kopi za kitabu hicho na kupatikana katika maktaba kuu zote hapa nchini pamoja na kwenye mitandao ya kijamii.

Kitabu hicho kimezinduliwa wakati Watanzania wanaadhimisha Miaka 61 ya Mafanikio ya Muungano wa Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here